Habari za Kitaifa

Kaunti kulipa Naibu Gavana wa zamani Sh5.7 milioni kwa kutopewa nyumba

Na JOSEPH WANGUI September 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Mahakama ya Mahusiano ya Kazi imetangaza kuwa manaibu wa magavana wana haki ya kulipwa marupurupu ya nyumba iwapo hawana makazi rasmi au nyumba iliyopangishwa na serikali ya kaunti yao.

Katika uamuzi wa kihistoria wenye athari kubwa kifedha, Jaji Onesmus Makau alithibitisha uamuzi wa mahakama ya hakimu uliompa aliyekuwa Naibu Gavana wa Kirinyaga, Peter Ndambiri, Sh5.7 milioni kama marupurupu ya makazi, akisema mwongozo wa Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kuhusu suala hilo ni wa kisheria na lazima utekelezwe.

Uamuzi huo, ambao unaweza kusababisha kaunti kupata madai ya mamilioni, unatokana na mgogoro wa muda mrefu kati ya Bw Ndambiri na serikali ya kaunti ya Kirinyaga.

Kesi hiyo pia inaonyesha changamoto zinazowakabili manaibu wa magavana, hasa baada ya mizozo ya kisiasa na viongozi wao wa kaunti.

Jaji Makau alisema miongozo iliyotolewa na SRC mwaka 2017 na 2019, inayotaka kaunti ziwape manaibu magavana marupurupu ya makazi, ni sharti la kisheria.

Alisisitiza kuwa manaibu magavana wanastahili marupurupu hayo kama watumishi wengine wa serikali, akirejelea uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba ulisema kuwa kunyimwa marupurupu hayo ni ubaguzi na kinyume cha katiba.

Suala kuu lilikuwa iwapo Bw Ndambiri alipaswa kulipwa marupurupu ya nyumba moja kwa moja, huku serikali ya kaunti ikidai hakutoa ushahidi kuwa alikuwa akiishi kwenye nyumba ya kupanga alipokuwa akihudumu (2017-2022).

Hata hivyo, mahakama ilisema serikali ya kaunti iliposhindwa kumpa makazi rasmi au nyumba iliyopangishwa kama ilivyopendekezwa na SRC, haikuondoa haki yake ya kulipwa Sh90,000 kila mwezi kwa kipindi chote alichohudumu.

Bw Ndambiri alihudumu kutoka 2017 hadi 2022 akiwa chini ya Gavana Anne Waiguru.

“Nakubaliana kuwa miongozo ya SRC kuhusu marupurupu ya nyumba kwa watumishi wa serikali za kaunti na manaibu wa magavana ya Agosti 25 2017 na Mei 20 2019 si mapendekezo tu, bali ni miongozo ya kisheria inayotakiwa kufuatwa,” alisema Jaji Makau alipokataa rufaa iliyowasilishwa na serikali ya kaunti dhidi ya uamuzi wa mahakama ya hakimu.

Manaibu wengine wa magavana waliodai haki zao ni pamoja na Caroline Karugu (Nyeri) na Hillary Chongwony (Bungoma)