Upinzani kutaja jina la muungano na viongozi wake
VINARA wa upinzani wametambua majina matatu yanayozingatiwa ya muungano mpya wa kisiasa kuelekea katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Kulingana na taarifa kutoka kwa kamati ya kiufundi inayosimamia mchakato huo, majina yaliyopendekezwa ni: Muungano wa Ukombozi, Komboa Kenya Alliance, na Mageuzi Coalition. Jina la nne – Liberation Alliance Movement – lilikataliwa kwa kuwa linafanana sana na chama cha People’s Liberation Party kinachoongozwa na Martha Karua.
“Majina haya yamechaguliwa baada ya mashauriano ya wiki kadhaa kwa lengo la kupata chapa itakayovutia Wakenya waliokatishwa tamaa na hali ya sasa ya kisiasa na kiuchumi,” alisema afisa mmoja wa kamati hiyo ya kiufundi.
Majina hayo yanawakilisha maono ya mabadiliko, ukombozi na mshikamano, na yanachukuliwa kama hatua muhimu katika kujenga nguvu ya kisiasa ya upinzani kitaifa.
Muungano huo unajumuisha viongozi mashuhuri kama vile Rigathi Gachagua wa DCP, Kalonzo Musyoka (Wiper), aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa, kiongozi wa Democratic Party (DP) Justin Muturi na Martha Karua wa PLP.
Kamati hiyo pia imepanga kikao cha faragha ili kushughulikia mvutano kuhusu nani atakuwa mgombeaji wa urais kwa niaba ya muungano huo, na pia kupitisha rasmi jina na maafisa wa muungano.“Sekretarieti imeomba viongozi wa muungano huo kuidhinisha jina na maafisa wa muungano ili shughuli zianze rasmi,” mdokezi akaeleza.
Bw Wamalwa alithibitisha kuwa kikao hicho kitafanyika hivi karibuni: “Tunaandaa kikao cha kupanga masuala ya muungano. Kitakuwa hivi karibuni,” alisema.
Hata hivyo, hatua hii inajiri wakati Rais William Ruto, kwa usaidizi wa kiongozi wa ODM Raila Odinga, akiongeza mashambulizi ya kisiasa dhidi ya upinzani, akiwataka kueleza ajenda yao kwa Wakenya badala ya “porojo zisizo na maana”.
“Hatutaruhusu vitisho wala shinikizo kutoka kwa ‘wantam’. Tunajua wapi tunaipeleka nchi hii,” alisema Rais alipokuwa akizindua mpango wa uwezeshaji katika Kaunti ya Nairobi.Uamuzi wa jina la muungano wa upinzani unatarajiwa kuathiri pakubwa taswira ya kisiasa ya kambi hiyo na namna utakavyopokelewa na wananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Kamati ya kiufundi imesisitiza umuhimu wa kuafikiana kwa maridhiano ili kuzuia mgawanyiko unaoweza kudhoofisha muungano huo.
“Ni lazima tupate mgombeaji anayeweza kuvutia kura kutoka maeneo yote ya nchi na kushindana na chama tawala kwa ufanisi,” alisema mmoja wa wanakamati.Wachambuzi wa kisiasa wanasema jina litakalochaguliwa litaashiria mwelekeo wa muungano huo – iwe ni katika muktadha wa ukombozi, mageuzi, au mshikamano wa kitaifa.
Uamuzi huo pia utakuwa na uzito mkubwa kwa wapigakura, na utasaidia kufafanua sura ya kisiasa ya Gachagua baada ya kutofautiana na Rais Ruto.Ikiwa viongozi wa muungano huo wataafikiana, kuweka ajenda wazi kwa taifa, na kuendeleza siasa za masuala badala ya migogoro ya ndani, basi wana nafasi ya kuwa mpinzani mkuu wa serikali katika uchaguzi wa 2027.
Hata hivyo, bila umoja wa kweli, huenda wakaishia kugawanyika kama miungano mingine ya awali.