Jamvi La Siasa

Wakenya wasubiri ‘Uhuru angurume’

Na BENSON MATHEKA September 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BAADA ya kimya cha muda mrefu, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta anatarajiwa kurejea jukwaani kisiasa kupitia Mkutano Maalum wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) wa chama cha Jubilee, unaotarajiwa kufanyika Ijumaa, Septemba 26, 2025.

Mkutano huo umepewa uzito mkubwa kisiasa, huku baadhi ya wachanganuzi wakiutaja kama wa ‘Uhuru kukohoa’ ishara ya mwanzo mpya katika siasa za upinzani na huenda pia ukawa onyo kwa wale waliokuwa wameanza kusahau ushawishi wake.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, anasema kuwa Uhuru atatumia jukwaa hilo kutoa mwelekeo wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Kauli hii imeibua hisia tofauti miongoni mwa Wakenya na wanasiasa wa pande mbalimbali, huku wengi wakingoja kwa hamu kusikia atakachosema.

Swali kuu linalozunguka vinywani mwa wengi ni iwapo Uhuru Kenyatta anarudi tena katika mstari wa mbele katika siasa za Kenya.

Ingawa amekuwa kimya tangu kuondoka madarakani mwaka wa 2022, hatua yake ya kuitisha mkutano wa NDC na kutarajiwa kuhutubia wanachama wake ni dalili za ushawishi wake katika siasa hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Wafuasi wake wanaamini bado ana mtaji mkubwa wa kisiasa, hasa katika maeneo ya Mlima Kenya na sehemu nyingine alikojijengea heshima kama kiongozi wa kitaifa.

Kioni anathibitisha hili akisema: “Kiongozi wetu wa chama ndiye atakayetuhutubia. Hajazungumza nasi kwa muda mrefu kwa sababu tulikuwa na kesi za kuokoa chama kisiibwe. Tungetaka atueleze anavyotaka tuendeshe chama hiki kuelekea 2027.”

Lakini kurejea kwake kunaweza pia kuibua changamoto. Baada ya kuondoka mamlakani, sehemu ya viongozi wa Jubilee walihama chama hicho na kujiunga na Kenya Kwanza.

Hivyo, wengi wanasubiri kusikia mwelekeo atakaotoa hasa kuhusu waliojaribu kumpokonya chama.

Kwa mujibu wa Kioni, lengo kuu la mkutano huo ni kuthibitisha kuwa Jubilee bado ni chama thabiti, kiko rasmi katika upinzani, na kimejipanga kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa 2027.

Pia, atawakaribisha wagombeaji wapya wanaotaka kuwania nyadhifa mbalimbali kwa tikiti ya Jubilee.

“Tunataka kuwaambia wafuasi wetu wa Jubilee kwamba tumekuwa kwenye kampeni tukisema ‘Ruto lazima aende.’ Tulikuwa pia tukipambana mahakamani kuhakikisha chama hakikuibwa. Sasa tumemalizana na hizo kesi za kortini,” alisema Jeremiah Kioni.

Mbunge huyo wa zamani wa Ndaragwa alisema Uhuru atatoa hakikisho kwa wanachama kwamba kiko katika upinzani.

“Atathibitisha kuwa tunatumia Jubilee na kwamba kila mmoja wetu yuko upande wa upinzani, ili watu waache kututilia shaka.”

Mkutano huo unajiri kukiwa na tetesi kuwa Uhuru anapanga kumkabidhi aliyekuwa waziri katika serikali yake Fred Matiang’i uongozi wa Jubilee aweze kutumia kugombea urais katika uchaguzi wa 2027.

Bw Kioni, amekuwa akifafanua mara kwa mara kuwa chama kitamuunga Matiang’i kugombea urais dhidi ya William Ruto.

Bw Matiang’i hajatangaza chama atakachotumia kugombea urais japo anakiri anatambua Jubilee iliyompatia nafasi ya kuhudumu serikalini katika nyadhifa tofauti za uwaziri.

Bw Matiang’i amekuwa akishirikiana na viongozi wengine wa upinzani Kalonzo Musyoka, Rigathi Gachagua, Martha Karua, Justin Muturi na Eugene Wamalwa.

Iwapo Jubilee itarejea kwa nguvu chini ya uongozi wa Uhuru, huenda ikaibua msisimko katika upinzani na kuufanya thabiti kumenyana na Kenya Kwanza.

Wachanganuzi wanasema iwapo Uhuru atatangaza wazi kushirikiana na viongozi wengine wa upinzani au hata kumpa Matiang’i usukani wa Jubilee inavyosemekana, kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka kwa muungano mpya wenye nguvu kuelekea 2027.

Licha ya matumaini hayo, changamoto zinabaki kuwa nyingi.

“Kwanza, ni lazima Uhuru aeleze wazi ikiwa anarejea katika siasa kama mshauri au mlezi wa chama. Uamuzi huo utasaidia kuweka wazi nafasi yake na kuepusha mkanganyiko wa uongozi.

“Pili, chama kinahitaji kushughulikia tofauti zilizopo ndani ya uongozi wake, hasa kati ya wale waliobaki waaminifu kwa Uhuru na wale waliotangulia kutangaza utiifu kwa serikali iliyopo. Pia, itabidi kifanye kazi ya ziada kujijenga katika maeneo ambayo ushawishi wake umepungua,” asema mchanganuzi wa siasa Dorothy Nerima.