Ni hatari kutumia vifaa bebe kama yaya dijitali
Wazazi wengi wanapoteza vita dhidi ya teknolojia. Vifaa bebe vimekuwa sehemu ya kawaida ya maisha yetu ya kila siku. Ni jambo la kawaida kuwaona watoto wadogo wakitumia simu, iPads, na hata televisheni.
Kuanzia kuzaliwa, watoto hutambulishwa kwa vifaa hivi kuwaburudisha na kuwanyamazisha. Katika mazingira mengi ya kijamii, wazazi mara nyingi hutegemea vifaa hivi kuwapumbaza na kuwanyamazisha watoto wao.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watoto wachanga na wadogo zaidi hawapaswi kabisa kutumia vifaa hivi hadi wafikishe umri wa miaka miwili, na watoto walio chini ya miaka mitano hawapaswi kutumia vifaa hivi kwa zaidi ya saa moja kwa siku.
Hili linakinzana kabisa na tamaduni za kisasa, jambo linalowafanya wazazi wahisi kama wanapigana vita ngumu. Hata hivyo, wataalamu wanaonya wazazi wasilegee katika majukumu yao na kuruhusu teknolojia kulea watoto wao.
“Mimi ni mzazi wa watoto sita, na ninaelewa vishawishi vya kutumia teknolojia kama “yaya ya kidijitali.” Faida moja inayoonekana ni kuwa wazazi huhisi wana udhibiti zaidi wa mahali alipo mtoto na wanaweza kuhakikisha usalama wao wa kimwili. Ikiwa mtoto anatazama iPad chumbani au sehemu nyingine ya nyumba, bado yuko karibu na anaonekana. Teknolojia huwavuta watoto kwa ufanisi kiasi kwamba mara nyingi hubaki sehemu moja, jambo linalopunguza hofu ya hatari za nje,” asema mtaalamu wa malezi dijitali Belton Theresa.
Anasema ingawa hii huonekana kama njia salama, ni lazima wazazi watambue kuwa matumizi kupita kiasi ya vifaa hivi yanaweza kudhuru maendeleo ya kiakili na kihisia ya mtoto, ambayo ni muhimu sawa na afya yao ya mwili.
Utafiti unaonyesha kuwa matumizi ya vifaa hivi kupita kiasi huathiri vibaya nidhamu binafsi, udadisi, uwezo wa kutekeleza majukumu, uthabiti wa kihisia, na hata ujuzi wa kijamii. Zaidi ya hayo, watoto hukosa usingizi wa kutosha, jambo ambalo pia huathiri ukuaji wao.
Kwa maneno mengine, dhana kuwa vifaa hivi ni salama kwa malezi kiasi cha kutumiwa kama yaya dijitali haiungwi na ukweli wa kisayansi.
Sababu nyingine inayowafanya wazazi kutegemea vifaa hivi ni hitaji la kupumzika au kushughulikia majukumu mengine.
“Ninalielewa hilo kabisa; ni rahisi zaidi kuwasha televisheni au kumpatia mtoto iPad kuliko kumtumbuiza kila wakati. Lakini suluhisho si kutumia vifaa hivi kubeba mzigo wa kuwatumbuiza watoto kila saa. Watoto wanapaswa kujifunza kukubali hali ya kuchoka. Kuchoka huchochea ubunifu, huimarisha afya ya akili, na huongeza ujuzi wa kijamii. Kuwafundisha watoto kustahimili kimya na kutafuta njia za ubunifu kuingiliana na mazingira yao ni jambo muhimu kwa maendeleo yao,” asema Belton.
“Wazazi hawapaswi kuruhusu maisha rahisi, utamaduni au faraja kuwaongoza katika malezi yao,” aongeza