Makala

Adhabu za makosa ya kufanya mapenzi na watu wa familia

Na  BENSON MATHEKA September 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Katika jamii ya Kiafrika, familia ni taasisi takatifu inayojengwa kwa misingi ya heshima, maadili na ulinzi kwa kila mwanachama.

Hata hivyo, vitendo vya baadhi ya wanafamilia kuvunja mipaka ya uhusiano wa damu kwa kufanya mapenzi na ndugu wa karibu vimeibua taharuki na kuhuzunisha jamii. Sheria ya Kenya inatambua kitendo hiki kuwa ni kosa la jinai na imeweka adhabu kali kwa wanaotenda kosa hilo.

Kwa mujibu wa sheria, mwanaume yeyote anayefanya kitendo cha aibu au kitendo kinachosababisha kupenya sehemu za siri za mwanamke ambaye ni binti yake, dada yake, mama yake, mjukuu wake, shangazi, mpwa au bibi yake, akifahamu kuwa huyo ni jamaa yake wa damu, huwa anatenda kosa. Adhabu ya kosa hili ni kifungo kisichopungua miaka kumi gerezani.

Hali huwa mbaya zaidi iwapo msichana aliyefanyiwa kitendo hicho ana umri wa chini ya miaka kumi na minane. Katika hali hiyo, sheria inasisitiza kuwa mtuhumiwaatafungwa kifungo cha maisha, bila kujali iwapo kitendo hicho kilifanyika kwa idhini ya msichana huyo. Hii ni kwa sababu sheria inalenga kulinda watoto dhidi ya unyanyasaji wa kingono.

Aidha, mtu yeyote anayejaribu kufanya tendo la ngono na mtu wa familia yake waliye na uhusiano wa damu hata  bila kufanikiwa, anahesabiwa kuwa ametenda kosa la jaribio la kushiriki tendo la ngomo na mtu wa  familia na anaweza kuhukumiwa kifungo cha angalau miaka kumi akipatikana na hatia.

Mbali na adhabu ya kifungo, mahakama ina mamlaka ya kisheria kumpokonya mtu huyo haki yoyote ya kuwa mlezi au msimamizi wa mtoto aliyeathiriwa. Mahakama pia inaweza kuteua mlezi mwingine kumlinda mtoto huyo hadi atakapofikisha umri wa utu uzima.

“Mwanamume yeyote atakayepatikana na hatia kwa kosa lolote chini ya kifungu hiki au jaribio la kutenda kosa hilo, mahakama itakuwa na uwezo wa kutoa amri zinazojulikana kama “amri za kifungu cha 114” chini ya Sheria ya Mtoto, 2001 (Sheria Na. 8 ya 2001) na pia kumvua mtuhumiwa mamlaka yoyote juu ya mwanamke huyo, kumwondoa katika uangalizi wake, na kuteua mtu au watu wengine kuwa walezi wa mwanamke huyo hadi atakapofikisha umri wa utu uzima au kwa kipindi kifupi zaidi kama itakavyoelekezwa,”

Kwa ujumla, kushiriki tendo la ngono na mtu wa familia si kosa tu la kisheria bali pia ni doa kubwa la kimaadili. Ni wajibu wa kila mzazi, mlezi na mwanajamii kulinda heshima ya familia na kuhakikisha kuwa watoto na jamaa wa damu wanalindwa dhidi ya maovu ya aina hii. Wanaotenda makosa haya si tu wanavunja sheria, bali pia wanavunja mioyo na kuharibu maisha ya watu wasiostahili kuteseka.