Habari za Kaunti

Wamiliki 3,800 wa ardhi ya Keekonyokie wapatiwa hatimiliki baada ya miaka 50

Na STANLEY NGOTHO September 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Takriban wanachama 3,800 wa ardhi ya jamii ya Keekonyokie, ambayo imekuwana utata kwa muda mrefu, hatimaye wamepokea hati miliki zao binafsi baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka 50. Hili limejiri huku kukiwa na mvutano mkali kati ya Wizara ya Ardhi (Ardhi House) na serikali ya kaunti ya Kajiado.

Ardhi hiyo ya jamii ya thamani ya  100 bilioni iko katika eneo la Kibiko, Kaunti Ndogo ya Kajiado Magharibi, na ina ukubwa wa ekari 2,800.

Kagawanywa kwa ardhi hiyo kulikuwa kumesitishwa kwa zaidi ya miaka 13 kutokana na migogoro ya uongozi kati ya makundi mawili yanayopingana – kundi linaloongozwa na mwenyekiti wa muda mrefu Moses Parantai na lile lingine linaloongozwa na Moses Monik.

Mnamo Julai 2025, Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Kajiado iliamuru Moses Parantai kuwasilisha hati miliki asili ya ardhi ya Kibiko mahakamani ndani ya saa 72. Aidha, Jaji L. Komingoi aliamuru kuwa iwapo Parantai atashindwa kutii, Msajili Mkuu wa Ardhi atoe cheti mbadala cha umiliki wa ardhi nambari LR No. Ngong/Ngong 12418 kwa jina la Moses Maseko Monik na wafuasi wake. Kundi la Parantai lilikata rufaa kupinga agizo hilo.

Mchakato wa kuchapisha hati miliki kwa ardhi hiyo ambayo tayari ilikuwa imeshapimwa ulianza, na sasa hati zinatolewa kwa wanachama bila malipo, kwa awamu.

Moses Monik, amepuuza madai kuwa hati hizo zilitolewa kwa njia za udanganyifu, akisisitiza kuwa Wizara ya Ardhi ilitekeleza maagizo ya mahakama kikamilifu.

“Tunatoa hati hizi kwa wanachama wetu bila upendeleo wowote. Katika awamu ya kwanza, wanachama 3,868 wamepokea hati miliki zao. Serikali iligharamia  hati hizi,” alisema Monik siku ya Jumamosi akiwa ameandamana na mamia ya wanachama. “Hizi ni hati halali zilizotolewa na Wizara ya Ardhi kwa mujibu wa sheria. Maneno ya wapinzani si ya kweli.”

Walionufaika wa mpango huo walielezea  afueni kubwa, huku wakisema kuwa hatua hiyo ni ishara ya haki na uwazi katika usimamizi wa ugavi wa ardhi hiyo kwa wanachama halali.

“Ugawaji wa ardhi ya Kibiko ulikuwa umechelewa mno. Angalau wanawake sasa wanamiliki ardhi kwa majina yao. Mimi sasa ni mmiliki halali wa ardhi,” alisema Bi Alice Lasoi kwa furaha.

Kundi la Mosoni liliahidi kuwa wanachama wote walioko kwenye sajili watapokea sehemu yao ya ardhi, huku waliokwisha jenga au kuishi kwenye maeneo fulani wakipangiwa ardhi hiyo hiyo waliyoitumia. Inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya ardhi hiyo tayari imejengwa na ina wakazi, hasa ikipakana na Kaunti ya Kiambu.

Hata hivyo, hatua hii mpya imezua mvutano kati ya Idara ya Ardhi ya Kaunti na Wizara ya Ardhi (Ardhi House), huku kila upande ukitupiana lawama.

Mnamo Ijumaa, Waziri wa Kaunti (CECM) wa Ardhi na Mipango ya Matumizi ya Ardhi Hamilton Parseina aliibuka na kudai kuwa ugawaji wa ardhi ya Kibiko ni wa udanganyifu, na kwamba mahakama zinatumika kama njia ya kufanikisha ufisadi katika sekta ya ardhi.

“Walaghai ni maafisa wa serikali walioko Ardhi House. Hati hizi za udanganyifu zinachapishwa katika kituo cha utoaji hati kilichoko Ruaraka na kisha kupelekwa Ardhi House ili zipelekwe kwa walengwa, wengi wao wakiwa si wenyeji na kampuni binafsi,” alisema Parseina wakati wa mkutano na wanahabari Kajiado.

Parseina alidai kuwa hati hizo zilianza kutayarishwa Agosti 28 2025 hadi Septemba 15 2025 lakini tarehe hizo zilibadilishwa hadi Julai 14 2025 kwa lengo la kukwepa agizo la Mahakama ya Rufaa lililotolewa  Julai 16 2025.

“Kaunti haijawahi kutoa idhini yoyote ya mipango ya matumizi ya ardhi (PP2) wala hatujapokea fomu yoyote ya PPS1. Mchakato huu hauna baraka za kaunti,” aliongeza.

Aidha, Parseina alisema kuwa alimtumia ujumbe wa maandishi Waziri wa Ardhi Bi Alice Wahome mnamo Agosti 28, 2025 kuhusiana na sakata hiyo, lakini hajapokea majibu hadi sasa.

“Ni jambo la kusikitisha sana kuona maagizo ya mahakama yanakiukwa waziwazi na maafisa wa serikali. Wanasiasa wakuu wakiwemo maseneta na wabunge wanahusika katika sakata hili kwa manufaa yao binafsi. Tutawataja hadharani hivi karibuni,” alisema Parseina.

Mbali na sakata ya Kibiko, Parseina alitaja visa vingine vya unyakuzi wa ardhi nchini ikiwemo msitu wa Ololua, eneo la Ngong Hills, ardhi ya mifugo Ngong, Torosei, Olodonyonyokie, Rombo, Mailua, Mbirikani na mashamba ya pamoja ya Kuku Group Ranches