Mikakati ya ODM kulinda umaarufu 2027
CHAMA cha ODM kinaonekana kulenga kujiimarisha baada ya kuanza misururu ya mikutano ya kujivumisha kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 tangu kianzishwe.
Baada ya kutua kwa kishindo Wajir wikendi, ODM itaandaa mikutano yake mingine katika kaunti za Mombasa na Kilifi ambayo itakuwa kilele cha maadhimisho hayo.
Kinara wa ODM Raila Odinga, Rais William Ruto na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi pamoja na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ni kati ya viongozi waalikwa kwenye sherehe ya ODM Mombasa kati ya Oktoba 10-12.
Ijumaa hii, viongozi wa ODM watakuwa mjini Kisii kama sehemu ya maadhimisho hayo.
Huku ikiwa dhahiri kuwa ODM itaingia kwenye muungano na UDA 2027, chama hicho kinamakinika kulinda ngome zake za kisiasa ili kisalie na idadi ya juu ya viongozi waliochaguliwa.
“Hatufai kutetereka kuhusu msimamo wetu wa kufanya kazi na serikali. Kiongozi wetu amekuwa mtu wa msimamo. Hii ndiyo maana chama hiki kimedumu kwa miaka 20 na kina wanachama kote nchini,” akasema Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga katika mkutano wa wikendi Wajir.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Naibu Kiongozi wa chama Abdulswamad Nassir ambaye pia ni Gavana wa Mombasa, Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed, Gavana wa Garissa Nathif Jama na mwenzake wa Wajir Ahmed Abdullahi, wabunge na viongozi wa nyanjani.
Bi Wanga alisema kwamba chama hicho bado kinamakinikia kutwaa mamlaka kama chama binafsi au kupitia muungano na vyama vingine.
“Kupigania haki za raia, ugatuzi na heshima kwa haki za kibinadamu ni kati mambo ambayo yamefanya tuwe imara kwa miaka 20 sasa,” akaongeza Bi Wanga.
Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna naye alisema chama hicho kitaendelea kupigania demokrasia na uongozi bora.
“Kama chama tumekuwa katika mstari wa mbele kuheshimu na kuzingatia Katiba. Nachukua fursa hii kuwaalika wafuasi wetu kwenye shughuli zetu na wakati huo huo kusisitiza kwamba chama hakijapoteza malengo yake,” akasema Bw Sifuna.
ODM inaadhimisha miaka 20 wakati ambapo kumekuwa na mgawanyiko mkubwa kati ya viongozi wake kuhusu uamuzi wa kushirikiana na serikali.
Pia chama hicho kitapambana kusalia imara kwenye ngome zake hasa eneo la Gusii na Magharibi ambako kinakabiliwa na maasi.
ODM pia inamakinika kushirikisha vijana katika shughuli zake huku umri wa kiongozi wake Bw Odinga, miaka 80 ukionekana kusonga.