Habari za Kitaifa

Kindiki mwokozi wa Ruto serikali ikianza kuimarika na kuwa thabiti

Na JUSTUS OCHIENG September 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU wa Rais, Prof Kithure Kindiki amegeuka kuwa mwokozi wa utawala wa Rais William Ruto, hekima yake ikiokoa serikali na kuonekana kuimarisha utendakazi wake.

Hii ni kinyume na jinsi aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ambaye alitajwa kuandama siasa za ubabe.

Wiki jana, Rais Ruto alimsifu Prof Kindiki hadharani akisema kuwa elimu yake ya juu imesaidia utawala wake kuwa thabiti.

“Nilikuwa na mwingine aliyekuwa analalamika, hajasoma, haha, nikaona ataniangusha,” Rais akaambia mkutano wa walimu katika Ikulu ya Nairobi.

Akimwangalia naibu wake, Rais aliongeza, “Huyu naibu wangu mnamwonaje, ni noma si noma, ni fire si fire. Unajua ukitaka kufaulu unatafuta naibu aliyesoma kuliko wewe.”

Wadadisi wa kisiasa wamemrejelea Prof Kindiki kama mwanasiasa mnyenyekevu ambaye hana ushindani wa kisiasa na anamakinikia kuchapa kazi serikalini.

Wametaja hatua zilizopigwa kwenye oparesheni za kiusalama na pia mageuzi ya kiuchumi kama zilizotokana na hekima ya Prof Kindiki ndani ya serikali.

“Ili Rais awe na mageuzi ndani ya serikali yake, lazima pawepo na usawa unaohitajika kutekeleza miradi na kupiga siasa,” akasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Douglas Mokua.

Duru zimearifu kuwa hekima ya Prof Kindiki imekuwa ikionekana hata kwenye mikutano ya Baraza la Mawaziri na mikutano mingine ambapo sera thabiti za kiuchumi huhitajika kukwamua serikali.

Elimu yake kama wakili wa masuala ya kikatiba pia imesaidia kung’amua jinsi serikali inavyoweza kukwepa mategu ya kisheria inapotekeleza miradi mbalimbali.

Baada ya kuapishwa kama naibu wa rais Novemba mwaka jana kutokana na kutimuliwa kwa Bw Gachagua, Prof Kindiki amegeuka mwanasiasa ambaye kwa sasa anaaminiwa sana na Rais kuelekea siasa za 2027.

Ndiye sasa anaongoza shughuli za kitaifa na kutetea miradi ya serikali wakati ambapo siasa za 2027 nazo zimeanza kuchacha.

Wakati wa kuapishwa kwa Prof Kindiki, Rais alikiri kuwa alihitaji naibu ambaye anafahamu sheria na ana elimu ya juu ili kumsaidia kutekeleza miradi ya serikali na ahadi ambazo zimefanikishwa.

“Nimekuwa mpweke hasa katika urais, nikipigia debe mipango na miradi ya serikali. Una ufasaha ndugu yangu, una hekima na nina imani utayaleta yale niliyokosa kupata kwa muda wa miaka miwili iliyopita,” akasema Rais.

Profesa Kindiki amegeuza makazi yake ya Irunduni, Kaunti ya Tharaka Nithi kama makao ya kuwapokea wanasiasa, raia ili kuwafahamisha kuhusu ajenda ya serikali na miradi.

Aidha ndiye sura ya mikutano ya kuinua makundi ya akina mama maeneo mbalimbali ambako huandamana na viongozi wengine kisha kutetea serikali.

Naibu Rais anaonekana analenga sana kuhakikisha Rais Ruto anasalia na kura za Mlima Kenya Mashariki baada ya kuonekana kuasiwa na mrengo wa Bw Gachagua Mlima Kenya Magharibi.