Raila aonya wabunge wa ODM dhidi ya kufanyia Ruto kampeni za 2027
KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga amewaonya wabunge wake dhidi ya kumfanyia Rais William Ruto kampeni 2027 akisema ODM bado ina nafasi ya kuwasilisha mwaniaji katika kura hiyo.
Kwenye tukio la kushangaza, Bw Odinga aliwaambia wabunge wa ODM wasome yaliyomo kwenye makubaliano yake na rais aliyosema hayazungumzi uchaguzi wa 2027.
“Bado hatujapitisha chochote kuhusu jinsi ambavyo uchaguzi wa 2027 utakavyokuwa. Kwa hivyo msiwekee chama masuala mengine ambayo hayajadiliwa,” akasema Bw Odinga.
“Wacha mambo hayo yajadiliwe kwanza. Sisi ni ODM, nani aliwaambia ODM haitakuwa na mwaniaji 2027?” akauliza.
Waziri huyo mkuu wa zamani alisema kuwa kama ODM msimamo wa chama kuhusu uchaguzi huyo ni jambo ambalo litajadiliwa baadaye.
Alikuwa akiongea jana wakati wa mkutano wa Kundi la Wabunge wa ODM.
Kauli yake ilikuja wakati ambapo wandani wake hasa kutoka eneo la Luo Nyanza wamekuwa wakirindima ngoma ya ‘Tutam’.
Wakati wa kikao hicho, ODM pia ilitathmini njia ya kujiondoa kwenye Serikali Jumuishi, wimbo ambao umekuwa ukiimbwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna.
Kulikuwa na wasilisho ambalo lilionyeshwa wabunge ambalo lilisema kuwa yaliyomo kwenye muafaka wa Ruto na Raila yasipotimizwa basi ODM iko huru kuondoka Serikali Jumuishi.
Aidha wasilisho hilo liliwakumbusha wanachama kuwa kwa kuingia kwenye Serikali Jumuishi, ODM haikupoteza mamlaka na utambulisho wake.
Kwa hivyo, Kenya Kwanza ilionywa kutotumia mikakati yoyote kisiasa kupuuza ODM na kuisawiri kama chama ambacho hakitakuwa na mwaniaji 2027.
Mkutano huo pia uliafikiana kuwa ODM itaitia mizani serikali kuhusu miswada, bajeti na teuzi mbalimbali ambazo zinafanywa nje ya sheria.
“Kamati za ODM lazima ziwasaili walioko serikalini hasa kuhusu masuala yaliyomo kwenye muafaka wetu na hayajatatuliwa,” akasema Bw Odinga.
Kauli ya Bw Odinga sasa inawaweka wabunge wa chama hicho katika njia panda kuhusu ushirikiano wao na serikali.
Hii ni kwa sababu Raila mwenyewe hapo awali amenukuliwa akisema kuwa yupo tayari kushirikiana na Rais hata 2027.
Aidha viongozi wengi kutoka ngome yake ya Nyanza, Pwani na Magharibi wameshasema Ruto tosha 2027 huku ikionekana wazi Bw Odinga hatawania urais kwa mara ya sita kutokana na ukongwe wake.