Bintiye Rais aondoa kesi dhidi ya mchapishaji
MWANAWE Rais William Ruto, Charlene jana alikubali kuondoa kesi aliyowasilisha mahakamani dhidi ya mchapishaji na mwandishi Webster Ochora Elijah.
Hatua hiyo sasa inalenga kuondoa utata wa kisheria ulioibua ghadhabu za umma kuhusu utambulizi na haki ya uchapishaji pamoja na sheria ya kidijitali.
Kiongozi wa mashtaka Esther Musinya jana alithibitisha kuwa kesi hiyo imeondolewa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Milimani Robinson Ondieki.
Wakili wa mchapishaji huyo Evans Ondieki alimkabidhi Bi Mutisya barua iliyoonyesha nia ya kuondolewa kwa kesi hiyo.
“Nathibitisha kwamba upande wa kiongozi wa mashtaka umepokea ombi la kuondolewa kwa kesi dhidi ya Bw Ochora. Nakala ya makubaliano yamewasilishwa kortini na nahitaji muda wa kupata amri ya korti kuhusu hili,” akasema Bw Mutisya.
Bw Ochora ameshtakiwa kuwa siku na kabla ya Mei 22, 2025 akiwa pamoja na watu wengine wasiokuwa mahakamani na eneo ambalo halijajulikana alijiwasilisha kama Charlene Ruto kwa kutumia akaunti ya matbaa inayofahamika Zawadi Publishers.
Alikamatwa na makachero kutoka DCI mapema mwaka huu na akafikishwa mahakamani ambapo aliwaachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 au pesa taslimu Sh50,000.