Habari

Diwani wa Githurai kujiuzulu Novemba 1, asema utawala wa Sakaja umemuangusha

Na KEVIN CHERUIYOT September 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

DIWANI wa wadi ya Githurai Deonysias Mwangi Waithira ametangaza kuwa atajiuzulu kufikia Novemba 1, akisema anahangaishwa na utawala wa Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.

Bw Mwangi alisema kuwa utawala wa Bw Sakaja hautekelezi miradi ya maendeleo kwenye wadi yake.

Bw Mwangi ambaye alichaguliwa kupitia UDA mnamo 2022 alisema uamuzi wake unatokana na uongozi duni wa Bw Sakaja ambao haufai hata maeneo mengine.

Alifunguka na kusema kuwa kwa kweli alikuwa amepanga kujiuzulu lakini barua ikaonekana na umma kabla hajaitia saini.

“Nilikuwa nimeamua kujiuzulu jinsi ambavyo imenakiliwa kwenye barua na niseme nitafanya hivyo Novemba 1, 2025. Hata hivyo, watu ambao wataamua mustakabali yangu ni watu wa Githurai,” Bw Mwangi akasema kwenye kipindi cha Fixing the Nation kinachopeperushwa na NTV.