MAONI: Viongozi wa kidini wakome kuelekeza waumini wao kuunga wanasiasa fulani
KATIKA kidemokrasia kama ya Kenya, uhuru wa kisiasa na uhuru wa dini ni misingi muhimu inayopaswa kuheshimiwa na kulindwa.
Hata hivyo, kumeibuka mjadala kuhusu nafasi ya viongozi wa kidini katika siasa, ambapo baadhi yao wamekuwa wakielekeza waumini wao kuhusu viongozi wa kisiasa wanaofaa kuunga mkono.
Hili ni jambo linalohitaji kuangaliwa kwa makini kwani linaweza kuhatarisha mwelekeo wa kisiasa wa taifa.
Kwanza, viongozi wa kidini wana ushawishi mkubwa kwa waumini wao kwa sababu ya heshima wanayopewa kama watu wa kiroho.
Wanapojihusisha moja kwa moja na siasa au kupigia debe wanasiasa fulani, huwaweka waumini katika hali ngumu ya kuchagua kati ya imani yao ya kidini na msimamo wao wa kisiasa.
Hii inaweza kuharibu misingi ya uhuru wa kuchagua na haki ya mtu binafsi kufanya maamuzi ya kisiasa bila shinikizo.
Pili, dini inapaswa kuwa chombo cha kuleta mshikamano, kukuza maadili, na amani katika jamii.
Viongozi wa dini wanapochukua misimamo ya kisiasa, mara nyingi hujenga migawanyiko miongoni mwa waumini, hasa katika maeneo yenye ushindani wa kisiasa.
Badala ya kuunganisha, viongozi hawa huweza kuwa chanzo cha chuki, uhasama, na hata migogoro ya kijamii.
Tatu, kuna hatari ya kupotosha ujumbe wa kidini kwa manufaa ya kisiasa. Wanasiasa wasio waaminifu wanaweza kutumia majukwaa ya dini kuwahadaa wananchi, wakijificha nyuma ya uaminifu wa waumini kwa viongozi wa dini.
Hili linaweza kudhoofisha maadili ya uongozi na kupunguza imani ya wananchi kwa taasisi za kidini.
Kwa hivyo, ni muhimu kwa viongozi wa kidini kuacha waumini wao kufanya maamuzi binafsi kisiasa. Wakenya wanapaswa kufanya maamuzi yao kwa kuzingatia sera, maadili, na uwezo wa viongozi, si kwa misukumo ya kidini.
Viongozi wa kidini nao wanapaswa kubaki kuwa waangalizi wa maadili katika jamii na sio kupigia debe wanasiasa makanisani.
Raia nao wanafaa kujua kupuuza viongozi wa kidini wanaohubiri siasa za upendeleo na kujua ujanja wa wanasiasa wa kutumia viongozi wa kidini.