Dembele alivyoshinda Ballon d’Or licha ya kuvurugwa na majeraha awali
BAADA ya kuvurugwa na majeraha mara kwa mara miaka ya hapo awali, hatimaye Ousmane Dembele ametimiza ndoto yake ya miaka mingi baada ya kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora Duniani katika tuzo ya Ballon d’Or, mbele ya Lamine Yamal, 18, wa Barcelona ambaye aliibuka mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa umri mdogo.
Aitana Bonmati wa klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania alitwaa tuzo hiyo kwa upande wa wanawake, hii ikiwa mara ya nne mfululizo.
Lionel Messi na Michel Platini ndio pekee waliowahi kushinda tuzo hiyo kwa miaka mitatu mfululizo.
Akipokea tuzo hiyo, Dembele alishindwa kuzuia machozi huku akiwashukuru jamaa na familia yake kwa kujitolea kwao kuboresha maisha yake.
Ilikuwa taswira halisi ya safari ngumu kuanzia chini, akapitia changamoto za kila aina kabla ya kufikia kilele Jumatatu usiku.
Dembele amefaulu miaka minne baada ya kauli ya aliyekuwa kocha wa Barcelona, Xavi Hernandez kubashiri mnamo 2021 kwamba siku moja staa huyo atakuwa mchezajhi bora duniani.
Hata kiungo huyo mshambuliaji aliyesajiliwa na Barcelona mnamo 2017 akitokea Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa ada ya Sh16 bilioni na kuwa mchezaji wa pili ghali zaidi duniani nyuma ya Neymar kwa muda mrefu hakuamini ubashiri huo wa kiungo huyo mstaafu.
Akisakatia Barcelona, Dembele alikosa utulivu kutokana na maswali kuhusu nidhamu na mtazamo wake, lakini kuimarika kwake kumemwezesha kutimiza unabii wa Xavi, ndoto aliyongojea kwa miaka mingi.
Dembele alianza polepole akiwa Barcelona, lakini aliimarika zaidi alipohamia PSG mnamo 2023 chini ya kocha Luis Enrique aliyempa majukumu mapya ya kufunga mabao.
Aling’ara vilivyo msimu uliomalizika wa 2024-25 akiwa na Paris Saints-Germain (PSG) akiisaidia klabu hiyo ya Ligue 1 bila Kylian Mbappe na kutwaa mataji matatu makubwa: Ligue 1, Coupe de Franc na UEFA Champions League, mbali na kufika fainali ya Kombe la Dunia na kushindwa na Chelsea.
Kwa jumla, staa huyo mwenye umri wa miaka 28 alifunga mabao 35 na kutoa pasi za mabao 14, na kutajwa kuwa mshambuliaji bora zaidi barani Ulaya kuanzia mwanzo wa mwaka.
Kwa mara ya kwanza katika taaluma yake, alizidi viwango vya mastaa kama Mohamed Salah wa Liverpool, Kylian Mbappe (Real Madrid), Lamine Yamal na Raphinha Dias (wote wa Barcelona).
Msimu uliopita, kocha Enrique alimwambia anataka mabao mengi pamoja na mchango mkubwa kutoka kwake, huku akimpa uhuru wa kuwa mchoyo kwa kutoa pasi na mwenye ari ya kufunga mabao, mawaidha ambayo yalimfanya afaulu binafsi pamoja na timu nzima.
Msimu wa 2023-24 alichezewa upande wa kulia sana kwa vile hakuwa na uwezo wa kumzidi Mbappe kama mshambuliaji wa kati.
Tangu Mbappe aondoke, Dembele alipewa nambari tisa, na amekuwa akifurahia nafasi hiyo ya kupokezwa mipira na kupata nafasi nyingi za kufunga mabao.
Kwenye halfa hiyo ya kufana iliyofanyika katika ukumbi wa Teatre du Chatelet jijini Paris, kocha Sarina Wiegman wa timu ya taifa ya Uingereza wa timu ya wanawake na Enrique wa PSG walitwaa tuzo za makocha bora, wakati Gianliuigi Donnarumma aliyechezea PSG msimu ulopita walitwaa na Emiliano Martinez wakiibuka makipa bora.