Habari za Kaunti

Wavinya akumbusha Rais Ruto apeleke miradi Ukambani

Na SAMMY KIMATU September 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Machakos Wavinya Ndeti ameitaka Serikali Kuu kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kaunti yake na eneo lote la Ukambani, akisisitiza kuwa serikali yake imekuwa ikishirikiana kikamilifu katika kuwezesha mipango hiyo.

Akizungumza Jumapili katika kaunti ndogo ya Masinga, gavana alifichua kwamba ofisi yake imetenga ardhi kwa ajili ya ujenzi wa masoko ya kisasa, imewasilisha orodha kamili ya miradi ya barabara iliyokwama kwa wizara husika kando na kudumisha mazingira mazuri ya ushirikiano kati ya serikali za ngazi mbalimbali.

“Tumeonyesha uaminifu wetu kwa kutoa msaada wote unaohitajika,” alisema Gavana Wavinya.

“Mpira sasa uko kwenye uwanja wa serikali kuu kutimiza ahadi zao kwa wananchi.”

Wakati huo huo, gavana alizindua mashindano ya tatu ya Kombe la Gavana Wavinya, akiwahakikishia vijana zawadi kubwa na kategoria mpya katika mchuano wa mwaka huu.

“Kombe la Wavinya sio tu kuhusu ushindani – bali ni kuwapa vijana wetu njia ya kujikwamua,” alisema, akiyataja malengo matatu makuu ikiwemo kutambua na kukuza vipaji vya vijana, kuimarisha umoja wa kijamii na kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia michezo.

Gavana alimtaja mkimbiaji Beatrice Chebet kwa mafanikio yake ya kushinda medali mbili za dhahabu kwenye mbio za mita 5,000 na 10,000 kwenye Michezo ya Olimpiki, akimtaja kuwa mfano kwa wasichana wengine.

“Ushindi wa Chebet unaonyesha yanayowezekana wakati kipaji kinakutana na fursa na uvumilivu,” alisema, akiwataka wasichana zaidi kujiunga na michezo.

Maombi ya gavana yanakuja wakati wakazi wa Ukambani wanaonyesha wasiwasi juu ya ucheleweshaji wa miradi ya kitaifa, fauka ya kuwepo kwa msaada wa ardhi na rasilimali kutoka kwa serikali ya kaunti.