Habari

Hofu mfanyabiashara akitekwa nyara ndani ya hospitali akitibiwa

Na NYABOGA KIAGE September 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MFANYABIASHARA mmoja wa Nairobi Mohamed Muktar kwa jina maarufu Gabun, 42, alitekwa nyara usiku wa Jumamosi, Septemba 20, na wanaume waliojidai kuwa maafisa wa polisi muda mfupi baada ya kuingia katika Hospitali ya Globe Care akiwa mgonjwa.

Bw Muktar, amekuwa akiugua shinikizo la damu kwa miaka mingi na kila anapozidiwa, huwa anakimbizwa hospitali hiyo iliyoko Barabara ya 11, Eastleigh, Kaunti ya Nairobi.

Wanaume waliodai kuwa polisi walimzuia, wakasimamisha matibabu yake na kumlazimisha kuingia kwenye gari aina ya Double Cabin Pick-up kisha kuondoka naye kwa kasi.

Utekaji huo ulifichuliwa na mfanyakazi mmoja wa hospitali hiyo ambaye anatoka Kaunti ya Wajir na ndiye aliyejulisha familia kuhusu tukio hilo.

Familia ilipoarifiwa, ilianza kumtafuta katika hospitali mbalimbali, vituo vya polisi na seli, lakini hakuna yeyote aliyekiri kumzuilia.

Kwa jamaa, marafiki na majirani, Muktar alitoweka ghafla.