Dimba

Wanabebwa kweli? Liverpool walivyopeleka ubabe wao Carabao Cup

Na REUTERS September 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MERSEYSIDE, UINGEREZA

LIVERPOOL iliendeleza ubabe wake msimu huu kwa kuwachapa Southampton mabao 2-1 katika mechi ya mchujo wa Carabao Cup, raundi ya tatu licha ya staa wao mpya Hugo Ekitike kulishwa kadi nyekundu.

Mshambuliaji huyo Mfaransa aliyenunuliwa kutoka klabu ya Eintracht Frankfurt aliadhibiwa baada ya kusherehekea bao lake kwa kuvua jezi, akisahau kuwa tayari alikuwa amepewa kadi ya njano.

Hatua hii itamgharimu staa huyo mwenye umri wa miaka 26 kwani hatakuwa katika kikosi mwishoni mwa wiki, The Reds watakapokutana na Crystal Palace, Jumamosi kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Nyota mpya Alexander Isak aliyesajiliwa kutoka Newcastle United kwa kitita cha Sh21.8 bilioni alifunga bao la kwanza dakika ya 43, likiwa lake la kwanza kufungia mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kabla ya Ekitike kuongeza la ushindi dakika ya 85.

Bao la Southampton lilifungwa na Shea Charles dakika ya 76 kutokana na makosa ya Wataru Endo.

Ulikuwa ushindi wa mechi saba mfululizo katika mashindano tofauti kwa Liverpool ambayo msimu uliopita walifika katika fainali na kupoteza kwa Newcastle United.

Kabla ya ushindi wa Jumanne usiku, Liverpoo ilikuwa imeshinda mechi tano za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na moja ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Kwenye mechi hiyo iliyochezewa Anfield, kocha Arne Slot alipumzisha mastaa 11 waliokuwa kwenye kikosi kilichoshinda Everton mwishoni mwa wiki ambao walicheza mechi tatu zilizopita na kumaliza dakika zote 90 katika kila mechi.

Kwingineko, Chelsea walikuwa jijini Lincolin katika uwanja mdogo wa LNER unaochukua mashabiki 10,000 na kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Lincoln City inayocheza kwenye Ligi ya Daraja ya Pili.

Ulikuwa ushindi muhimu kwa Chelsea ambao walianza msimu vizuri baada ya kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia miongoni mwa Klabu kabla ya kuanza kuandikisha matokeo ya mchanganyiko.

Matokeo hayo yamepunguza presha kwa kikosi hicho kutokana na matokeo ya hivi karibuni ikiwemo kufungwa 2-1 na Manchester United kwenye mechi ya EPL.

Katika mechi nyingine ya mashindano hayo ya Kombe la Ligi, Wolves waliwalaza Everton 2-0.

Kwingineko, Fulham walikuwa nyumbani kukaribisha Cambridge United na kuibuka na ushindi finyu wa 2-0, huku Brigton wakisafiri Barnsley na kurejea na ushindi mkubwa wa 6-0, wakati Burnley wakilimwa 2-1 na Cardiff City nyumbani.

Wrexham ya Daraja la Kwanza ambayo ilionekana kuja kwa kasi msimu uliopita ilishangaza tena baada ya kushindaa Reading 2-0.

Matokeo ya Carabao Cup:

Jumanne: Lincoln City 1-2 Chelsea, Wolves 2-0 Everton, Fulham 1-0 Cambridge United, Burnley 1-2 Cardiff City, Wrexham 2-0 Reading.