Dimba

Mogadishu City FC waomba msamaha kwa kukanyaga bendera ya Kenya

Na HILARY KIMUYU, JOHN ASHIHUNDU September 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TIMU ya Mogadishu City Club ya Somalia imeomba msamaha baada ya mashabiki wao wawili kuonekana wakidharau na kuidunisha bendera ya Kenya wakati wa mechi yao dhidi ya Kenya Police, mwishoni mwa wiki.

Wakati wa mechi hiyo ya mkondo wa kwanza wa mchujo wa Kombe la Mabingwa barani Afrika iliyochezewa Nyayo Stadium, mashabiki hao walionekana wakitembea na bendera ya Kenya huku wakiirusharusha, huku mmoja wao akionekana akiitumia kujipangusa nayo sehemu nyeti, kitendo kilichozua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii.

Tukio hilo liliwafanya Wakenya wengi kuanzisha kampeni ya kukabiliana vilivyo na Wasomali wanaoishi nchini kwa kukosea heshima taifa huru la Kenya.

Mashabiki hao walionekana kwenye video wakiikanyaga na kuitupa chini bendera hiyo kama kitambaa cha kawaida, kinyume na heshima yake.

Wakenya wa matabaka mbalimbali waliungana na mashabiki wa soka nchini, mashirika ya kiraia, na wandishi wa habari kukilaani kitendo hicho huku wakitaka wahusika wachukuliwe hatua kali za kinidhamu.

Wengi walikitaja kitendo hicho kama dharau kwa mamlaka ya Kenya, huku wengine wakisema ni kitendo cha kudhalilisha na kupuuza mamlaka ya Kenya.

Kwenye taarifa yake, klabu ya Mogadishu City Club ilijitenga haraka na tabia hiyo, na kukiita bahati mbayaisiyokubalika.

Klabu hiyo ilisema kitendo hicho kilitekelezwa na kundi dogo, wala hakiakisi maadili ya timu hiyo wala mashabiki wake kwa ujumla.

Kwa niaba ya Mogadishu City Club, tunashutumu vikali tukio hili na kutuma msamaha moja kwa moja kwa Serikali na wananchi wa Kenya.

“Tabia kama hii haifai kabisa kwenye mpira au katika moyo wa urafiki na uungwana katika mashindano.”

“Tutaunga mkono kikamilifu hatua yoyote itakayochukuliwa dhidi ya wahusika- na tunatoa mwito kwa mashabiki wetu, hasa wale wa umri mdogo, waheshimu mataifa yote, bendera zao, na watu wao.”

“Kandanda inakusudiwa kukuza umoja, upendo na kuheshimiana, mbali na kutumika kusuluhisha mizozo pamoja na kuleta watu pamoja.”

Miongoni mwa watu mashuhuri waliokilaani kitendo hicho ni pamoja na mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Nairobi, Esther Passaris aliyemtaka Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) kuwakamata na kuwafungulia mashtaka wahusika.