Makala

Korti yaagiza serikali kueleza iwapo afisa wa polisi Benedict Kabiru angali hai Haiti au la

Na RICHARD MUNGUTI September 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA Kuu imeagiza Mwanasheria Mkuu (AG) Dorcus Oduor atoe taarifa iwapo afisa wa polisi Benedict Kabiru aliaga dunia nchini Haiti ambako polisi wa Kenya zaidi ya 400 wanashika doria ili kudumisha amani.

Kabiru alikuwa katika ujumbe wa kwanza uliopelekwa kudumisha amani katika taifa hilo la visiwa vya Carribean ambako magenge hatari yanatawala.

Agizo la mahakama kwa Bi Oduor lilitolewa na Jaji Chacha Mwita baada ya kufahamishwa na wakili Mbuthi Gathenji kuwa Rais William Ruto alifichua Jumatatu wiki hii kwamba Kabiru aliaga dunia mnamo Machi 25, 2025.

Habari za kutoweka kwa Kabiru zilifichuliwa kwa mara ya kwanza na Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Douglas Kanja mnamo Machi 25 mwaka huu. Tangu wakati huo ni miezi sita ya kimya cha serikali.

“Miezi sita serikali ikiwa imenyamaza.Tumeshtushwa mno na tangazo la Rais Ruto – anayehudhuria kikao cha Umoja wa Mataifa (UN) – mjini New York, Amerika, kwamba Benedict Kabiru alifariki Machi 25,2025,” wakili Gathenji aliambia Jaji Mwita wakati wa kusikizwa kwa kesi ambayo familia ya Kabiru ilishtaki serikali.

Wakili huyo alieleza kwa masikitiko jinsi familia ya Kabiru imekuwa ikisaka habari kuhusu aliko jamaa wao.

“Muda huu wote tumeuliza serikali iwapo kumekuwa na mawasiliano kati ya Rais Ruto na baraza linaloongoza Haiti kuhusu Kabiru,” Bw Gathenji alidokeza.

Wakili wa serikali Betty Mwatsao aliomba siku saba kubaini ukweli kwani idara ya polisi imesema afisa huyo angali hai.

Wakili huyo aliambia Jaji Mwita kwamba afisi ya Mwanasheria Mkuu imeficha ukweli wa mambo kwa muda wa miezi sita sasa.

“Familia ya Kabiru imehuzunishwa na kifo cha mwanao kilichokuliwa kama siri na serikali,” Bw Gathenji alieleza korti.

Wakili wa serikali Betty Mwatsao aliomba muda wa siku saba abaini ukweli wa mambo kwa vile idara ya Polisi imesema kwamnba akali hai.

Jaji Mwita alishangazwa na msimamo wa serikali kuhusu aliko Kabiru.

“Naamuru Mwanasheria Mkuu awasilishe ripoti Oktoba 8,2025 kuhusu aliko Kabiru,” Jaji Mwita aliagiza.