Wito ‘wageni’ wasipewe nyumba za bei nafuu
AWAMU ya pili ya usajili wa nyumba za bei nafuu katika makazi ya mabanda ya Mukuru, Nairobi ilikamilika Alhamisi Septemba 25, 2025.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Ujenzi wa Nyumba za Bei Nafuu, Bi Sheila Mwaura, alisema jumla ya nyumba 4,500 zinatarajiwa kukabidhiwa rasmi kwa wanufaika na Rais William Ruto mwezi ujao.
“Awamu hii imekamilika na sasa tunasubiri hatua ya Rais kukabidhi nyumba hizo kwa wananchi,” akasema Bi Mwaura.
Hata hivyo, wakazi wa maeneo ya Mariguini na Mukuru wameitaka serikali kuhakikisha hakuna ubaguzi utakaofanywa wakati wa kukabidhi nyumba hizo.
Diwani wa Wadi ya Nairobi Kusini, Bi Waithera Chege, amewahimiza wakazi kuendelea kujisajili ili kufaidika na mradi huo na kuwataka kuepuka kuingiza siasa katika shughuli za maendeleo.
“Nawaomba wakazi wajitokeze kwa wingi kujisajili. Hii ni nafasi ya kubadilisha maisha yao, tusiruhusu siasa kuharibu mchakato huu,” akasema Bi Waithera.
Kwa upande wake, Mbunge wa Embakasi Kaskazini, Bw James Gakuya, ameitaka serikali kuhakikisha ni wakazi halali wa maeneo hayo pekee watakaonufaika na nyumba hizo.
“Mradi huu ni wa kubadilisha maisha ya wakazi wa Mukuru na Mariguini. Ni muhimu kuhakikisha wanaoishi hapa ndio wanapewa kipaumbele,” akasema Bw Gakuya.
Mradi wa nyumba za bei nafuu ni sehemu ya ajenda kuu ya serikali ya Kenya Kwanza ya kuhakikisha Wakenya wengi wanapata makazi bora kwa bei nafuu.
Zoezi la usajili ilianza Jumatatu wiki jana katika wadi ya Nairobi South likilenga takribani wakazi 2000 kutoka mitaa ya mabanda ya South B.
Serikali imetangaza kuwa kuanzia Januari mwaka ujao, itaanza kujenga na kupeana nyumba ya chumba kimoja na viwili katika awamu inayofuata ya mradi huo.