Waandamanaji wadai haki kwa mfanyakazi aliyeuawa kwa madai ya wizi wa Sh5,000
WAFANYAKAZI wa nyumbani, wanaharakati na wakazi wa Kibra wamefanya maandamano kutafuta haki kwa Bi Zaituni Kavaya, mama wa watoto wanne ambaye inadaiwa alikufa kwa kutupwa kutoka ghorofa ya tano na mwajiri wake katika mtaa wa Kilimani, Nairobi.
Kisa hicho kilikasirisha miungano ya wafanyakazi wa nyumbani kutoka mtaa wa Kibra wakitaka kufahamu jinsi mmiliki huyo alifikia hatua ya kusababisha kifo cha mwenzao.
Wakiongozwa na katibu wa muungano wa wafanyakazi wa nyumbani Bw Moses Shivairo, alisema kuwa walisikitishwa kufahamishwa kuwa marehemu alikuwa ameiba Sh5,000 kutoka kwa mwajiri wake na kujitia kitanzi.
Bw Shivairo alikana madai hayo akisema kuwa baada ya kifo cha marehemu, bintiye aliyechukua nguo za marehemu alikuwa na Sh160 pekee.
“Upasuaji wake ulifanywa na ukaonyesha marehemu alifariki kutokana na majereha ya kurushwa kutoka juu hadi chini sio kujitia kitanzi. Pia, mwanawe alipochukua nguo zake alipata Sh160 kwenye mfuko wake,” alisema Bw Shivairo.
Bintiye marehemu Faith Kavaya anasema anataka familia yake kupata haki kwa kuwa mamake aliuliwa kinyama na kuacha mzigo kwa familia.
“Tunataka haki itendeke mwenye alihusika akamatwe, maanake ametuacha sisi ni wadogo. Kuna ndugu zangu wadogo ambao walikuwa wanamtegemea. Alikuwa akilipa kodi ya nyumba sasa tutapata kujisaidia vipi na mimi sijajua maisha vizuri,” alisema Faith.

Kakaye marehemu Bw Bakari Mohammed anataka serikali kuweka masharti mapya ya kuwalinda waajiriwa wa nyumba kwa kuwa wengi wao hudhulumiwa na mabosi wao.
“Wakati umefika serikali isimame imara isikubalie watu wa nje kuangamiza watoto wetu ambao wanatafuta riziki kwa nchi yao. Huu ni unyanyasaji wa hali ya juu sana,” alisema Bw Mohammed.
Ripoti ya upasuaji iliyofanywa inaonyesha kuwa marehemu alifariki kutokana mshtuko pamoja na kupatikana sehemu zake za mwili zimevunjika. Hii ilitofautiana na ripoti ya polisi kuwa alijitia kitanzi.
“Huwezi kulinganisha maisha ya mtu na pesa. Mtu anafanya kitu kibaya, anakuhonga kisha unaandika ripoti mbaya. Wakati wa upasuaji nilikuwa na daktari na kuona sehemu zake zote za mwili ambazo zilikuwa zimevunjika. Daktari alisema dadangu alifariki kutokana na kuanguka kutoka sehemu ya juu,” alipiga kelele Bw Mohammed.
Kamanda wa polisi katika Kituo cha Kilimani Patricia Yegon alisema uchunguzi unaendelea akiwahakikisha wafanyakazi hao kuwa mwathiriwa atapata haki yake.
“Yangu ni kuwahakikishia kwamba tunaendelea na uchunguzi na Bi Zaitun atapata haki. Yule atapatikana kuwa alihusika atachukuliwa hatua kulingana na sheria… Kwa sasa watu wanne wanazuiliwa kwa sasa bado uchunguzi haujakamilika.”