Huko Carabao, wanyonge walinyongwa bila huruma
LONDON, UINGEREZA
Arsenal, Manchester City, Tottenham na Newcastle United zinazoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ziliingia hatua ya 16-bora ya kipute cha Carabao Cup baada ya kuwalemea wapinzani wanyonge kutoka ligi za chini nchini humo, Jumatano.
Mabingwa wa 1987 na 1993, Arsenal waliwalipua Port Vale 2-0, huku winga matata Bukayo Saka akianza kwa mara ya kwanza baada ya mapumziko ya wiki nne kutokana na jeraha la misuli ya paja.
Akifanya majukumu ya nahodha kutokana na kutokuwepo kwa Martin Odegaard, Saka alicheza dakika 63 kabla ya kupumzishwa.
Eberechi Eze alifunga bao la kwanza dakika ya nane kabla ya Leandro Trossard kuongeza la pili dakika ya 86.
Kocha Mikel Arteta alifichua kuwa kumpumzisha Saka kulikuwa tahadhari ya kuepuka majeraha zaidi.
Arsenal sasa watavaana na Brighton katika hatua ya kuingia robo-fainali.
“Inafurahisha kutwaa ushindi na pia bila kufungwa bao. Isitoshe, ilikuwa pia mechi ya kwanza ya kipa Kepa Arrizabalaga na nimefurahishwa naye sana,” akasema Arteta.
Mabingwa mara nane, Manchester City waliochezesha wana wa Emile Heskey, nyota wa zamani wa Uingereza na Liverpool, Jaden na Reigan, walipepeta wenyeji Huddersfield 2-0 ugani Kirklees.
Kocha Pep Guardiola alifanya mabadiliko tisa, lakini aliwacha Phil Foden na Savinho waliofunga mabao hayo.
Huddersfield waligonga mwamba mara moja, lakini City walidhibiti mchezo. Guardiola alisifu uthabiti wa safu ya ulinzi na nidhamu ya kikosi chake.
Tottenham Hotspur walioshinda Carabao kwa mara yao ya mwisho, na nne mwaka wa 2008, waliendelea na mwenendo mzuri chini ya kocha Thomas Frank walipolaza Doncaster 3-0 kupitia mabao ya Joao Palhinha, Jay McGrath (alijifunga) na Brennan Johnson jijini London.
Licha ya kufanya mabadiliko saba katika kikosi kilichocheza mechi iliyopita ya ligi, Spurs walitawala mchezo.
Palhinha anachezea Spurs kwa mkopo kutoka Bayern Munich.
Doncaster walitishia mara chache tu, lakini Spurs walisimama tisti.
Newcastle walianza vyema kutetea taji lao kwa kudidimiza viongozi wa Ligi ya Daraja ya Tatu, Bradford City, 4-1 uwanjani St James’ Park.
Joelinton na William Osula wa Newcastle walifunga mabao mawili kila mmoja. Andy Cook aliwapa Bradford bao la kufutia machozi.
Matokeo (Septemba 24): Huddersfield 0-2 Manchester City, Newcastle 4-1 Bradford City, Tottenham 3-0 Doncaster, Port Vale 0-2 Arsenal.
Droo ya 16-bora (Oktoba 28): Grimsby Town vs Brentford, Swansea vs Manchester City, Arsenal vs Brighton.