Uhuru aponda Gachagua kwa kutaka Matiang’i awe na chama kutoka Gusiiland
RAIS Mstaafu Uhuru Kenyatta amemkemea aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua kwa kushinikiza kuundwa kwa chama cha eneo la Mlima Kenya, akionya kuwa vyama vya kikabila au vya kikanda ni hatari kwa umoja wa kitaifa.
“Siasa ni kuhusu mapenzi ya pamoja ya watu, si maslahi madogo ya eneo,” alisema, kwa kauli iliyotafsiriwa kama ya kumshambulia Gachagua.
Bw Gachagua, kupitia chama chake Democracy for Citizens, amekuwa akijisawiri kama kiongozi wa eneo la Mlima Kenya na ametaka washirika wake katika upinzani kama aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kuunda chama cha kieneo badala ya kutegemea Jubilee.
Kenyatta pia alirudia mashambulizi ya kibinafsi yaliyomfuata baada ya uchaguzi wa 2022 na hata familia yake na mali yake kulengwa kwa makusudi.
“Nimepoteza na kushinda uchaguzi, na kila mara nimejifunza kuwa siwezi kuongozwa na chuki, hasira au uhasama. Hiyo hupotosha azma na maono yako,” alisema, akikumbuka uvamizi katika shamba lake la Northlands na uharibifu wa mali wakati wa maandamano ya mwaka jana.
Ingawa hakumtaja mtu yeyote kwa jina, wengi katika siasa wamekuwa wakimshutumu Gachagua kwa kuhusika na shambulizi hilo kama sehemu ya njama ya kuvunja ushawishi wa familia ya Kenyatta katika siasa za Mlima Kenya.
Bw Gachagua amekanusha madai hayo mara kwa mara.
Kenyatta pia alikosoa juhudi za Rais Ruto za kuunda “serikali jumuishi,” akilaumu serikali kwa kutumia migawanyiko ya kikabila na kieneo kama mbinu ya kujenga ujumuishaji wa kisiasa.
“Tulifanya kazi kama chama kuleta mshikamano mkubwa katika muundo wetu wa kijamii, kupunguza migogoro ya kikabila, na kushughulikia usawa wa kijamii na kieneo. Juhudi hii ilitumiwa dhidi yetu katika kampeni za mwisho na kuitwa jaribio la kudhoofisha demokrasia. Ninajiuliza wao leo wanaiita nini?” alisema huku akipigwa makofi.
Bw Kenyatta pia alikosoa jinsi serikali inavyoshughulikia masuala ya usalama, akiangazia hatari ya matumizi mabaya ya vyombo vya serikali kutisha wananchi.
“Tulihakikisha vyombo vyetu vya usalama vina uwezo wa kukabiliana na vitisho vya ndani na nje. Lakini tuliyojenga haikufaa kutumika kuwakabili raia wake wenyewe wala kuwa chanzo cha hofu na migogoro kati yao. Tunahitaji uongozi bora zaidi katika operesheni hizi,” alisema.
Maneno yake yalijiri wakati serikali ya Ruto inakabiliwa na ukosoaji mkali kuhusu tuhuma za utekaji nyara, matumizi mabaya ya vyombo vya usalama kuzima upinzani, na madai kuwa maafisa wa DCI wamekuwa wakifuatilia simu za wapinzani kwa kushirikiana na Safaricom.
Bw Kenyatta alitangaza kuwa “hataendi popote,” akiahidi kusimamia mwenyewe uteuzi wa wagombea wa chama na kuashiria nia ya Jubilee kuwania uchaguzi kote nchini huku ikishirikiana na watu wenye maono yanayofanana.