Habari za Kitaifa

Sonko apokea tuzo ya kimataifa kwa kusaidia maskini

Na NDUBI MOTURI September 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko, ametunukiwa tuzo tatu za heshima za kimataifa, zikiwemo Shahada ya Heshima ya Uzamifu katika Uongozi na Utawala Bora, kutokana na mchango wake katika maendeleo endelevu, kazi za kibinadamu na kijamii.

Shahada hiyo ilitolewa na Chuo Kikuu cha Amani na Utawala Bora cha Amerika (American University of Peace and Governance – AUPG, USA),  kutambua mchango wake katika sekta ya maendeleo na juhudi zake za kusaidia jamii.

“Angalia jinsi Mungu anavyoendelea kuniinua na kunifanikisha hata baada ya kutoka ofisini. Namrudishia utukufu kwa kuwa kazi yangu imetambuliwa kimataifa,” Sonko aliandika kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter).

Mbali na Shahada hiyo, Baraza Kuu la Umoja wa Kimataifa wa Amani na Utawala Bora (UNIPGC) lilimtunuku Sonko Tuzo ya Ubora wa Uongozi kutokana na uongozi wake wa mageuzi, uzalendo, na juhudi zake katika kukuza utawala bora.

Sonko pia alipewa heshima nyingine kupitia Mpango wa Uongozi wa Jewel Howard Taylor, mpango unaoendeshwa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Liberia.

Picha zilizoambatanishwa kwenye taarifa hiyo zilionyesha Sonko akipokea tuzo hizo Ijumaa, Septemba 26, wakati wa Kongamano la Uwekezaji na Amani la UNIPGC (GLISPA).

Katika taarifa yake Jumamosi, Sonko alisema alikuwa mwingi wa shukrani. “Jana, nikiwa pamoja na viongozi wengine kutoka mataifa mbalimbali duniani, nilipokea heshima hizi za UNIPGC katika Bunge la Uingereza.”

Aliongeza: “Nilitunukiwa Tuzo ya Ubora wa Uongozi kwa pamoja na Mpango wa Jewel Howard Taylor, pamoja na Shahada ya Heshima kutoka Chuo Kikuu cha AUPG cha Amerika, kutokana na mchango wangu mkubwa katika kazi za kijamii, misaada ya kibinadamu na ukuzaji wa rasilmali watu.”

Hafla hiyo ilifanyika katika jumba la kihistoria la House of Lords na liliandaliwa na tawi la Uingereza la UNIPGC, ikiwa ni sehemu ya toleo la tatu la kongamano la kimataifa la GLISPA.

Sonko pia alikuwa mzungumzaji mkuu katika mkutano huo, ambapo alisisitiza kuwa: “Uongozi wa kweli haupimwi kwa vyeo au nyadhifa, bali kwa athari chanya tunayoacha kwa binadamu.

“Uongozi bila huruma ni uongozi usiokamilika. Katika miaka yangu ya kuhudumu serikalini, nimejitahidi kwenda mbali zaidi ya siasa na sera, kwa kugusa maisha ya watu kwa njia halisi.”

UNIPGC hutambua na kutunuku taasisi na watu binafsi wanaochangia katika amani, maendeleo endelevu na uongozi bora duniani.

Tuzo hizi hutolewa kila mwaka katika kongamano maalum la kimataifa, warsha na vikao vya viongozi duniani kote.