IEBC sasa yaalika Gen Z kujisajili kama wapiga kura kuanzia Jumatatu
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inaanza rasmi zoezi la usajili wa wapiga kura kesho, Septemba 29, hatua ambayo huenda ikabadilisha mwelekeo wa Uchaguzi Mkuu wa 2027.
IEBC imetangaza kuwa inalenga kusajili wapiga kura wapya wasiopungua milioni 6.3, wengi wao wakiwa vijana waliotimu umri wa miaka 18 karibuni.
“IEBC inalenga kuongeza idadi ya wapiga kura kutoka milioni 22.1 hadi milioni 28.4 kufikia uchaguzi wa 2027 kupitia zoezi hili la usajili,” alisema Mwenyekiti wa tume hiyo, Bw Erastus Ethekon.
Zoezi hilo litaendeshwa kitaifa isipokuwa katika maeneo ambayo yana chaguzi ndogo, ambapo jumla ya chaguzi 24 zinatarajiwa kufanyika Novemba 27, 2025.
Bw Ethekon alisema zoezi hilo litawalenga zaidi vijana wa kizazi cha Gen Z, ambao wachambuzi wa kisiasa wanasema wanaweza kuwa na ushawishi mkubwa iwapo watajitokeza kwa wingi kusajiliwa na kupiga kura.
Profesa Tom Nyamache wa Chuo Kikuu cha Turkana alisema ikiwa vijana watajitokeza kwa wingi kujiandikisha na kupiga kura mwaka wa 2027, wataamua nani atakuwa rais wa sita wa Kenya. “Hii itakuwa mara ya kwanza uchaguzi kushindwa kwa misingi ya kizazi, si ukabila,” alisema.
Dkt Peter Mbae, mtaalamu wa masuala ya utawala, alisema vijana pia wataamua magavana, maseneta, wabunge na madiwani, iwapo watashiriki kwa wingi.
Mchambuzi wa kisiasa na wakili Steve Kabita aliongeza kuwa Gen Z wameonyesha hulka ya kisiasa isiyoegemea wanasiasa kikabila, na mara nyingi wamekuwa wakikosoa pande zote mbili-serikali na upinzani.
Kwa miaka miwili iliyopita, vijana wamekuwa wakiandamana kulalamikia hali ngumu ya maisha, ukosefu wa ajira, ushuru mkubwa na ukatili wa polisi. Lakini sasa, sauti yao huenda ikahitajika zaidi kwenye siasa rasmi.
Ripoti ya sensa ya 2019 inaonyesha kuwa kuna vijana milioni 17.8 wenye umri kati ya miaka 18–34, ambapo milioni 14 wanastahili kupiga kura 2027.
Katika uchaguzi wa 2022, IEBC ilisajili wapiga kura milioni 22.1, lakini ni milioni 14.3 pekee waliopiga kura. Takriban milioni 7.8 – wengi wao wakiwa vijana – hawakushiriki, hali iliyotajwa kama kiini cha kutoshiriki wapiga kura.
Uchaguzi huo uliamuliwa na tofauti ya kura 200,000 pekee – Rais William Ruto alipata kura 7,176,141 dhidi ya Raila Odinga aliyepata 6,942,930.
IEBC imesema huduma zitakazotolewa katika zoezi hili ni pamoja na usajili mpya, kusahihisha taarifa za mpiga kura, kuhamisha usajili hadi eneo lingine la uchaguzi, na kuthibitisha taarifa za mpiga kura.
Wananchi pia wanaweza kuthibitisha taarifa zao mtandaoni kupitia tovuti: verify.iebc.or.ke