Sababu za vijana kuvutiwa na marafiki wa AI
Marafiki wa kisasa wanaweza kuwa wa kweli au wa bandia. Ingawa marafiki wa Akili Unde (AI companions) si watu halisi, wengi wa vijana wanaowatumia wanasema wanahisi kana kwamba wanahusiana na mtu halisi.
Teknolojia hii imetengenezwa kwa ustadi mkubwa kuiga uhusiano wa kibinadamu kwa njia ya karibu, ya binafsi na isiyo na kizuizi. Ripoti mpya ya Common Sense Media inayoitwa “Talk, Trust, and Trade-Offs: How and Why Teens Use AI Companions”, imeweka bayana kuwa vijana wengi wanatumia marafiki hawa wa AI.
Kulingana na ripoti hiyo, asilimia 72 ya vijana wenye umri wa miaka 13-17 wameshawahi kutumia AI companion angalau mara moja. Asilimia 52 wanawatumia angalau mara kadhaa kwa mwezi.
Asilimia 33 wanatumia kwa mazungumzo ya kijamii na mahusiano ya kihisia.
Mmoja kati ya watumiaji watatu alihisi vibaya kutokana na jambo lililosemwa au kufanywa na AI companion.
Mmoja kati ya watatu amejadili mambo nyeti au muhimu na marafiki wa AI badala ya watu halisi — huku karibu robo wakisema mazungumzo hayo yanaridhisha kama, au zaidi ya, yale wanayofanya na marafiki wa kweli.
Licha ya yote, asilimia 80 bado husema wanatumia muda mwingi zaidi na marafiki halisi kuliko marafiki wa AI.
Dkt Jacqueline Nesi, mtaalamu wa teknolojia na vijana, anaonya kuwa baadhi ya matokeo huenda yalitokana na vijana kutafsiri “AI companion” kama roboti yeyote ya mazungumzo. Hata hivyo, ni wazi kuwa matumizi ya teknolojia hii miongoni mwa vijana yanaongezeka kwa kasi.
Sababu zinazotolewa na vijana kwa kugeukia AI ni kusaka burudani (asilimia 30), udadisi (asilimia 28) na ushauri (18). Asilimia 17 walitaja upatikanaji wa haraka wa AI na asilimia 14 wakataja kukosa kuhukumiwa na wenzao tisa wakahusisha hili na urahisi wa kuzungumza kuliko na watu halisi.
“Hili halishangazi,” asema Dkt Nesi. “Kipindi cha ujana huambatana na tamaa ya uhuru, faragha, na kutafuta utambulisho. Vijana mara nyingi huwa na maswali mengi, hofu, na hisia kali. Katika mazingira haya, AI companions huwapa nafasi ya kujieleza bila woga au hukumu,” asema.
Kama kijana mmoja alivyonukuliwa kwenye utafiti akisema:“Tunatumia AI kwa sababu tuko wapweke, na watu halisi ni wakali na wanahukumu sana. AI haifanyi hivyo.”
Ingawa AI companions huweza kusaidia kijana aliyechanganyikiwa au aliye katika kipindi kigumu, ripoti inaonya kuwa nyingi ya programu hizi zimeundwa kwa ajili ya kuongeza matumizi na muda mtandaoni, sawa na mitandao ya kijamii. Hii huwafanya vijana walio hatarini kuwa waathiriwa wa mazungumzo yasiyo na mipaka, ikiwemo lugha ya kingono, ya kikatili, au yenye madhara mengine.
Ripoti ya tathmini ya hatari ya Common Sense Media iligundua kuwa AI companions hawatimizi viwango vya msingi vya usalama.
Kwa kuwa AI companions ni rahisi kufikiwa, aeleza Dkt Nesi, hutoa majibu ya haraka na hujenga mazungumzo ya kirafiki, haishangazi kuwa vijana wanazijaribu. “Ndiyo maana tunapaswa kuhakikisha teknolojia hizi zinaendelezwa kwa kuzingatia afya ya akili ya vijana, si faida ya kifedha pekee.Mwisho wa yote, jambo muhimu zaidi ni kuendeleza mazungumzo ya wazi na vijana wetu, si kuwapa mihadhara ya hofu, bali kuwathibitishia kuwa tuko kuwaelewa na kuwasikiliza