Pambo

Kasirikia mpenzi wako kwa busara

Na BENSON MATHEKA September 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Katika kila uhusiano wa kimapenzi,iwe ni uchumba au ndoa, hisia za hasira hujitokeza mara kwa mara.

Hasira si tatizo. Ni hisia halali za kudhihirisha kuwa kuna jambo lisilo sawa. Lakini jambo la msingi si kuwa na hasira, bali namna ya kuelezea hasira bila kuvuruga, kuumiza, kudhalilisha na hata kuvunja uhusiano.

Kulingana na mwanasaikolojia Dkt Sue Johnson, mahusiano ya kina hujengwa si kwa kuepuka migogoro, bali kwa namna watu wanavyotatua migogoro hiyo kwa upendo.

Anasema watu wengi hukosea kwa kufikiri kuwa kuelezea hasira ni kutoa yote waliyo nayo bila kujali athari. Lakini kuna tofauti kubwa kati ya kuwa na hasira na kuwa katili. “Hasira ni hisia; ukatili ni chaguo la mtu. Ukikasirika, mweleze mwenzi wako ulivyohisi badala ya kumshambulia kwa maneno. kunyamazia hasira pia ni sumu. Usimnyamazie mwenzi wako ukidhani atajua mwenyewe kosa lake,” asema.

Mtaalamu wa mahusiano Dkt Gary Chapman, mwandishi wa kitabu cha The 5 Love Languagesanashauri kuwa njia bora ya kushughulikia hasira ni kwa mazungumzo ya wazi na ya upendo.”

Anasema huwa kwa sababu ya hasira, wapenzi huwa wanaanika matatizo yao kwa watu wa nje—marafiki, familia, au hata mitandaoni.

“Hili si suluhisho, bali ni kuongeza chumvi kwenye kidonda. Mahusiano yanahitaji nafasi salama ya makosa na uponyaji, si mahakama ya watu wa nje,” asema.

Mtaalamu wa mahusiano Bi Esther Perel, anasema kila mtu anafaa kulinda uhusiano wake. Kila uhusiano mzuri unahitaji uwezo wa kulinda heshima ya mwenzako hata wakati wa maumivu,” asema.

Kama umeumizwa, asema, kumbuka kuwa hata wewe umewahi kukosea na ukasamehewa. “Usiwe na tabia ya kukumbusha makosa ya zamani kila mnapogombana, hasa yale ambayo ulisema umesamehe. Usitumie hasira kama silaha ya kihisia, yaani, kunyima tendo la ndoa, kutumia watoto kama ngao, au kulipiza kisasi kwa usaliti,” ashauri.

Perel anasema watu hukosea kwa kutisha wachumba wao wakiwa na hasira. “Usitishie kuondoka kila mnapogombana. Kauli kama “nimechoka”, “hii ndoa haina maana”, au “tunaachana tu” zinapojirudia huwa mbegu ya hofu na kuondoa imani. Mahusiano imara yanahitaji ari ya kushughulikia matatizo, si kuyatoroka mradi hakuna dhuluma za kimwili,” asema.

Unapokasirika, asema Johnson,  jitahidi kuangalia mazuri ya mwenzi wako. Tambua kuwa bado huyo huyo ndiye uliyempenda, ambaye mlimcheka pamoja, mkaota pamoja, na mkaahidi kuwa pamoja hata mambo yakiwa magumu.

“Upendo wa kweli hujifunza kuvumilia hata wakati wa hisia kali.Na hata unapohisi huna nguvu ya kuzungumza, usiache kumuombea mwenzi wako. Maombi huleta upole wa moyo na neema ya msamaha. Kumbuka, hasira ni ya muda, lakini maneno mabaya yanaweza kuumiza maisha yote,” aeleza

Wataalamu wanashauri watu kukasirika, lakini kwa heshima. “Mnaweza kukosana, lakini hasira isiwe sababu ya kutengana. Ukiwa wa kutoroka kwa sababu ya kukasirika, hautaweza uhusiano wowote kwa kuwa hakuna malaika katika ulimwengu wa mapenzi. Utaumizwa na kukosewa na mtu unayempenda,” asema Perel.