Habari

Watu 13 wafariki katika ajali matatu ilipogongana na trela Gilgil

Na ERIC MATARA September 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WATU 13 walifariki dunia kufuatia ajali mbaya iliyohusisha matatu ya kubeba abiria 14 na trela Jumapili, Septemba 28, 2025 asubuhi katika eneo la Kariandusi, karibu na mji wa Gilgil, katika barabara kuu ya Nairobi-Nakuru.

Ripoti za awali zinaashiria kuwa ajali hiyo ilisababishwa na kugongana kwa magari hayo mawili, ambapo matatu iliharibika vibaya hasa sehemu ya mbele.

Trela, kwa upande mwingine, lilibingiria na kutumbukia kwenye mtaro kando ya barabara, jambo linaloonyesha kuwa dereva alishindwa kulidhibiti.

Wakazi wa eneo hilo walikimbilia eneo la tukio mara tu baada ya ajali, wakijaribu kutoa huduma ya kwanza kwa manusura huku vipande vya magari na mizigo mbalimbali vikitapakaa barabarani.

Ajali hiyo ilijiri saa chache tu baada ya ajali nyingine kutokea karibu na hapo, ambapo watu sita waliangamia Jumamosi jioni, miongoni mwao wakiwa ni wahudumu wa ambulensi.

Ajali hiyo ya pili ilitokea katika eneo la Kimende, ambapo gari la wagonjwa kutoka Hospitali ya St Mary’s Mission, Elementaita, lilikuwa likikimbiza mgonjwa mahututi hospitalini.

Walioshuhudia walisema gari hilo lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi kabla ya dereva kupoteza mwelekeo na kugonga kingo za barabara kwa nguvu.

Wote waliokuwa ndani, mgonjwa, mume wake, jamaa wawili, muuguzi na dereva walifariki papo hapo.

Katika kisa tofauti siku hiyo hiyo, ajali nyingine ilitokea katika barabara hiyo hiyo eneo la Gilgil, kati ya Kikopey na St Mary’s, na kuleta msongamano mkubwa wa magari.