Habari za Kitaifa

Wataalamu watoa sababu za ardhi kupasuka mara kwa mara Nakuru

Na BRYGETTES NGANA September 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WIKI mbili zilizopita, sehemu ya Barabara Kuu ya Nakuru-Eldoret ilipasuka ghafla na kuzama, na kuunda mashimo mawili makubwa, jambo lililosababisha msongamano mkubwa wa magari.

Tukio hili liliwaogofya wakazi na watumiaji wa barabara kwa sababu ardhi ilionekana kama inaweza kuporomoka wakati wowote. Hata hivyo, hii si mara ya kwanza tukio kama hili kutokea Nakuru.

Mwaka mmoja uliopita, ardhi ilizama katika eneo la Eveready Roundabout baada ya mvua kubwa kunyesha – tukio lililofanana sana na la hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Prof Simon Onywere wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, ardhi ya Nakuru iko juu ya miinuko ya krateri ya Menengai, eneo ambalo liliumbwa na mikwaruzo ya kihistoria ya kijiolojia ya Bonde la Ufa.

Prof Onywere anaeleza kuwa jiji la Nakuru limejengwa juu ya mistari mingi ya ufa ambayo kwa kawaida hufichwa na udongo mnene wa volkeno.

Hata hivyo, wakati mvua kubwa inanyesha, maji huingia katika nyufa hizo na kusababisha udongo wa juu kusombwa – hali inayofanya ardhi kuonekana kama inapasuka ghafla.

Mchakato huu unajulikana kama mmomonyoko wa chini ya ardhi ambapo mashimo ya ndani ya ardhi hujitokeza taratibu hadi kufikia hatua ya ardhi ya juu kusambaratika.

Hali hii imekuwa kawaida hasa baada ya mvua kubwa kunyesha, na imeonekana katika maeneo kama Mai Mahiu mwaka 2018.

Nakuru ina takriban mistari mitano ya ufa upande wa magharibi, na mitatu kati yake hupitia katikati ya jiji. Eneo la Barabara ya Nakuru-Eldoret – ambayo ni njia kuu ya kiuchumi kuelekea nchi jirani za Afrika Mashariki – pia imepitia juu ya nyufa hizi. Hili linafanya miundombinu kuwa katika hatari kubwa ya kupasuka kila mara mvua inaponyesha.

Prof Onywere anasema kuwa maeneo kama ya mizunguko ya barabara yaliyoathirika hapo awali yalijazwa kwa mawe na kifusi tu, badala ya kushughulikiwa ipasavyo kutoka chini kabisa ya ufa.

Anaonya kuwa suluhisho la muda mfupi halitoshi, na kwamba serikali inapaswa kuwekeza kwenye msingi imara wa ujenzi, ikiwemo kuweka nguzo za simiti hadi chini ya miamba ya ufa.

Ujenzi huu lazima ufanywe kwa kutumia utaalamu wa hali ya juu unaozingatia hali halisi ya kijiolojia ya eneo hilo.

Kwa sasa, hakuna idara ya serikali iliyofanya tathmini kamili ya kina na upana wa nyufa hizi ili kuzuia majanga yanayoweza kutokea.

Wataalamu pia wanaonya kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaongeza kasi ya uharibifu huu wa kijiolojia.

Hata hivyo, kuna habari njema huku wataalamu wakiondoa hofu kwa kusema kwamba Nakuru haizami, bali matatizo haya ni ya ndani ya ardhi na yanaweza kushughulikiwa kwa uhandisi wa kisasa na mipango bora ya matumizi ya ardhi.