Habari za Kitaifa

Kesi mpya kupinga Ushuru wa Nyumba yawasilishwa kortini

Na JOSEPH WANGUI September 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MASHIRIKA ya kutetea haki za raia na wananchi binafsi wamewasilisha kesi mpya mahakamani kupinga ushuru wa ujenzi wa nyumba, wakitaka utangazwe kuwa kinyume cha sheria.

Kesi hiyo ambayo imewasilishwa katika Mahakama Kuu jijini Nairobi, inalenga kukomesha utekelezaji wa mpango huo wa serikali ya Rais William Ruto.

Kwa mujibu wa walalamishi, ushuru huo unaokatwa kutoka kwa mishahara ya wafanyakazi walio kwenye ajira rasmi imegeuzwa kuwa chombo cha kisiasa cha kutafuta kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Wanasema kuwa Rais Ruto amekuwa akitumia ujenzi wa nyumba hizo kuwavutia wapigakura kwa kuzigawa kwa makundi maalum ya wataalamu kama walimu, maafisa wa usalama, na hata wachezaji wa timu ya taifa ya soka Harambee Stars, bila kufuata mchakato wa kisheria.

Mashirika yaliyopeleka kesi hiyo ni pamoja na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC), Transparency International Kenya, Inuka Kenya Ni Sisi, The Institute for Social Accountability (TISA), na Siasa Place.

Wanadai kuwa ushuru huo ni mzigo usio wa haki kwa wafanyakazi wanaolipa kodi, huku wengi wao wakiwa hawana nafasi ya kunufaika moja kwa moja na nyumba hizo.

Katika kesi hiyo, wamelalamikia kauli ya Rais ya kuagiza asilimia 20 ya nyumba hizo zitengewe walimu, na asilimia nyingine 20 kwa maafisa wa usalama bila idhini ya Bodi ya Ujenzi wa Nyumba Nafuu kama inavyotakiwa na sheria.

Wanasema hatua hiyo inakiuka usawa kikatiba na haki ya kupata makazi kwa Wakenya wote bila ubaguzi. Aidha, wanapinga madai ya serikali kuwa mradi huo umeongeza ajira na kukuza uchumi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Takwimu la Kitaifa (KNBS) ya mwaka 2024, sekta ya ujenzi ilipungua kwa asilimia 0.7, matumizi ya simiti yakashuka kwa asilimia 7.2, na uagizaji wa chuma pia ukapungua kwa asilimia 12. Ripoti hiyo pia inaonyesha kupungua kwa ajira katika sekta ya ujenzi kwa asilimia 4.2.

Huku serikali ikidai kuwa mradi huo unasaidia kukuza maendeleo, walalamishi wanasema hali halisi ni kwamba unazidi kuwaumiza raia wa kawaida, kupunguza uwezo wao wa kifedha, na kuongeza umaskini. Wanataja ushuru huo kama usiozingatia usawa.

John Maina na Marshalls Ongaya, walioungana na mashirika hayo katika kesi hiyo, wanasema kuwa mamilioni ya Wakenya wanaochangia ushuru huo hawajapewa nafasi sawa ya kunufaika na nyumba hizo, jambo linaloendeleza ubaguzi kinyume cha Katiba ya Kenya, kifungu cha 27.

Wanaomba mahakama isimamishe mara moja kukata ushuru huo na iutangaze kuwa ni kinyume cha Katiba.

Pia wanataka Bodi ya Nyumba Nafuu iandae mwongozo wa wazi, wa haki, na usio wa kibaguzi kuhusu usambazaji wa nyumba hizo.

Serikali bado haijajibu rasmi madai katika kesi hiyo mahakamani.