Raila bado ana nafasi ya kurejea Upinzani, asema Natembeya akijitenga na Kenya Moja
NAIBU Kiongozi wa chama cha DAP-Kenya, George Natembeya, amejitenga na vuguvugu la kisiasa la Kenya Moja, akisema kuwa halina azma ya kweli ya kukomboa Wakenya kutoka utawala wa Kenya Kwanza.
Akizungumza na Taifa Leo, Natembeya alikanusha madai kwamba yeye ndiye mwanzilishi wa mrengo huo unaoongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na Mbunge wa Githunguri Gathoni wa Muchomba, akisisitiza kuwa juhudi zake ziko ndani ya upinzani ulioungana unaolenga mabadiliko ya kweli kwa nchi.
“Sihusiki na Kenya Moja. Huo ni mrengo usio na maono ya pamoja. Kama kweli tunataka kuondoa utawala huu wa Ruto, hatuwezi kufanya hivyo kwa kugawanyika. Tunahitaji umoja wa kweli wa upinzani, si miungano ya kujaribu bahati,” alisema Natembeya.
Akikosoa kiongozi wa ODM Raila Odinga, Natembeya alisema hatua ya kumuunga mkono Rais William Ruto ni usaliti kwa Wakenya waliomwamini kama kiongozi wa mageuzi.
Alisema kuwa Raila anapaswa kurudi katika nafasi yake kama kiongozi wa upinzani.
“Raila bado ana nafasi ya kurejea upinzani. Heshima yake kisiasa iko hatarini ikiwa ataendelea kuwa sehemu ya serikali ya Kenya Kwanza. Hii si siasa ya maadili aliyojenga kwa miaka mingi. Kwa sasa anaonekana kama mtu anayejitafutia maslahi binafsi,” alisema.
Alisema kuwa Wakenya wanahitaji kiongozi atakayewakilisha masilahi yao bila kupotoshwa na vyeo au makubaliano ya kisiri serikalini.
Aliongeza kuwa juhudi zozote za kuunda miungano ya kisiasa nje ya mwongozo wa upinzani ulioungana ni baraka kwa Ruto na zitaleta mkanganyiko kwa wapinzani wa kweli wa serikali.
“Ni lazima tupate mgombea mmoja wa upinzani kupitia ushirikishaji wa wananchi. Si watu wachache tu wakae mahali na kuamua. Kenya Moja ni vuguvugu lisilo na uthabiti wa kisiasa, na kama hawataungana nasi, basi wanafanya kazi ya Ruto bila wao kujua,” alisema.
Kwa sasa, Natembeya anashikilia kuwa yeye ni sehemu ya upinzani halisi unaoongozwa na viongozi wengine kama vile Rigathi Gachagua (DCP), Kalonzo Musyoka (Wiper), Martha Karua (PLP), Dr Fred Matiang’i, Eugene Wamalwa (DAP-K) na Justin Muturi (DP).