Habari za Kitaifa

IEBC yasema imeweka mikakati tele Gen Z kujiandikisha kwa kura kuanzia leo

Na DAVID MWERE September 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeweka wazi mikakati kabambe ya kuhakikisha inasajili wapiga kura wapya milioni 6.3 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027, licha ya baadhi ya wabunge kuonyesha wasiwasi kuhusu kufikiwa kwa lengo hilo.

Hatua hii inajiri huku IEBC ikizindua rasmi shughuli ya usajili wa wapiga kura leo katika Kaunti ya Kajiado.

Shughuli hii inakadiriwa kugharimu walipa ushuru takriban Sh7 bilioni, kwa lengo la kuongeza idadi ya wapiga kura kutoka milioni 22.1 waliokuwa wamesajiliwa kufikia uchaguzi wa 2022.

Kulingana na Mwenyekiti wa IEBC, Bw Erastus Ethekon, tume itaweka pia mikakati ya muda maalum ya usajili wa wapiga kura kabla ya uchaguzi, ili kuongeza idadi ya wanaojiandikisha.

“Tutatumia mbinu zote za mawasiliano, hasa kupitia mitandao ya kijamii, kuhamasisha vijana ambao hawajasajiliwa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vya usajili katika vyuo vya elimu ya juu,” alisema Bw Ethekon.

Shughuli ya usajili itafanyika katika ofisi za tume za maeneobunge, isipokuwa maeneo 24 ya uchaguzi ambayo yanajiandaa kwa uchaguzi mdogo wa Novemba 27, 2025.

Bw Ethekon alisema takwimu za wapiga kura wapya wanaolengwa zilichukuliwa kutoka kwa mashirika ya serikali ya kitaifa kama Shirika la Takwimu la Kitaifa (KNBS) na Idara ya Usajili wa Watu (NRB), ambazo zinaonyesha Wakenya waliotimiza umri wa miaka 18 lakini hawajasajiliwa kupiga kura.

Aidha, alibainisha kuwa asilimia 70 ya wapiga kura ni vijana na ni muhimu kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa sababu “huu ni wakati wao”.

“Tume tayari imetangaza maafisa wa usajili na wasaidizi wao kisheria, kama msingi wa utekelezaji na uwajibikaji,” alieleza Bw Ethekon.

Mbunge wa Suba Kusini, Bw Caroli Omondi, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Uangalizi wa Utekelezaji wa Katiba (CIOC), alieleza wasiwasi kuhusu jinsi IEBC itafikia lengo hilo la wapiga kura wapya milioni 6.3, akisema uungwaji mkono wa kisiasa pia ni muhimu.

“Nina mswada unaopendekeza vitambulisho vya kitaifa kutolewa shuleni kwa wanafunzi wa sekondari ili kuwawezesha vijana kupata vitambulisho mapema na kujiandikisha kupiga kura,” alisema Bw Omondi, huku Mbunge wa Tiaty, William Kamket akiongeza, “je, lengo hilo linaweza kufikiwa kweli?”

Chini ya Sheria ya Usajili wa Watu, kitambulisho ni hati muhimu ya uraia kwa walio na miaka 18, inayohitajika katika kupiga kura na kupata huduma za serikali na nyingine kama kufungua akaunti ya benki.

Katiba ya Kenya katika Kifungu cha 38(3) na 83 inatambua haki ya kila raia aliyehitimu kujiandikisha kupiga kura, huku Kifungu cha 88(4) kikiitaka IEBC kuhakikisha utekelezaji wa usajili endelevu wa wapiga kura.

Licha ya hayo, IEBC haikufanya hivyo baada ya uchaguzi wa 2022 kwa sababu haikuwa na makamishna wapya hadi Julai 11, 2025, baada ya waliotangulia kuondoka Januari 2023 walipokamilisha muhula wao wa miaka sita.

IEBC, baada ya kuundwa upya, ilitangaza Septemba 29, 2025 kuwa tarehe rasmi ya kuanza tena kwa zoezi hilo.

Kamishna wa IEBC, Bi Anne Nderitu, ambaye anaongoza kamati ndogo ya elimu ya wapiga kura, alisema tume imekamilisha tathmini ya kina ya vituo vya usajili na iko tayari kutangaza maeneo 27,000 kama vituo rasmi vya usajili.

“Ni muhimu vijana wa Kenya wanaofikia umri wa kupiga kura waelimishwe kuhusu haki yao ya kikatiba ya kushiriki uchaguzi,” alisema Bi Nderitu.

Bi Nderitu aliongeza kuwa tume ina kamati maalum ya kushughulikia masuala ya vijana, ambayo itapewa ufadhili kwa ajili ya kushirikiana na taasisi zote nchini zinazohudumia vijana, iwe ni za serikali au za kibinafsi, kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu haki yao ya kupiga kura.

IEBC inatumia takwimu za sensa kupanga malengo ya usajili kwa kutathmini idadi ya watu wanaotarajiwa kufikia umri wa kupiga kura kufikia mwaka wa uchaguzi.