MAONI: Rais asikilize ushauri wa Uhuru, arudishe ‘Linda Mama’ na ‘Edu Afya’
WANDANI wa Rais William Ruto wamekasirishwa na hatua ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kukosoa baadhi ya sera zilizoanzishwa na serikali ya Kenya Kwanza katika sekta mbalimbali.
Viongozi kama Seneta wa Nandi Samson Cherargei wanafaa kumpongeza Bw Kenyatta kwa kujitokeza na kutaja dosari zinazoumiza raia ikizingatiwa amewahi kukalia kiti anachokalia Dkt Ruto sasa.
Rais huyo wa zamani alisema ukweli ni kwamba, hali sio shwari katika sekta za afya, elimu, usalama na uchumi kwa ujumla.
Kauli ya Bw Kenyatta imetiliwa uzito na matokeo ya hivi punde ya utafiti ulioendeshwa na kampuni ya Infotrak yaliyoonyesha kuwa,asilimia 57 ya Wakenya wanahisi kuwa taifa linaelekea mkondo mbaya.
Walitaja kupanda kwa gharama ya maisha, ukosefu wa ajira, kukithiri kwa ufisadi, usimamizi mbaya wa bima ya afya miongoni mwa changamoto zingine kama kiashirio kuwa hali sio shwari.
Isitoshe, viongozi wa Kanisa la Kianglikana Nchini (ACK) wamejitokeza na kulalamikia changomoto zinazokumba sekta muhimu za elimu na afya wakiitaka serikali ya Ruto kurekebisha hali katika nyanja hizo.
Kwa hivyo, kabla ya Bw Cherargei, na wenzake, kumkaripia Bw Kenyatta wakidai “aliharibu nchi”, wafungue macho na masikio yao waone na kusikia madhila ambayo wagonjwa wanapitia kutokana na utendakazi mbaya wa Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA) inayosimamia bima ya afya ya kijamii (SHIF).
Bw Kenyatta haenezi propaganda zisizo na mashiko anaposikitika kuwa utawala huu umevuruga mpango aliouanzisha wa Linda Mama.
Chini ya mpango huo, akina mama wajawazito walipata huduma za kujifungua bila malipo.
Lakini sasa, serikali inadai kuwa mpango huo umeshirikishwa katika bima ya SHIF ambayo kwa karibu mwaka mmoja sasa utekelezaji wake umekumbwa na changamoto.
Hii ina maana kuwa, akina mama wamekuwa wakiteseka kwa muda huo tangu kuzimwa kwa “Linda Mama” hali inayochangiwa na SHA kuchelewa kutoa pesa kwa hospitali zilizosajiliwa kutoa huduma chini ya bima hiyo.
Kwa upande mwingine, ninahisi kuwa serikali ilikosea ilipoondoa mpango wa Edu Afya ambao uliwahudumia wanafunzi wa shule za upili za umma wakati wa utawala uliopita.
Nyakati hizo, serikali ilikuwa ikitenga angalau Sh4 bilioni kila mwaka kugharamia matibabu ya wanafunzi. Mpango huo haukushirikishwa na iliyokuwa Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF).
Kwa hivyo, wandani wa Rais Ruto wanaoshutumu Bw Kenyatta kwa kukosoa bima ya sasa ya afya wajue kuwa kiongozi huyo anazingatia ukweli wa hali ilivyo.