Vidume Phoenix na vipusa wa KU wang’aa katika Roll Ball
TIMU ya wanaume ya Phoenix na wanawake wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) kila moja ilianza kwa vyema kampeni za ligi kuu ya Roll ball kwenye mechi zilizochezewa uwanja wa Gretsa University, mjini Thika Jumapili, Septemba 28, 2025.
Wanaume wa Phoenix chini ya kocha Danson Lingati ilipepeta Chuka University kwa mabao 9-2 nao vipusa wa KU walizaba GOA mabao 2-0.
Kitengo cha wasichana KU chini ya nahodha, Sandra Osongo ilipata ushindi huo kupitia juhudi zake Wanjiku Githinji na Jecinta Mwangi waliofunga bao moja kila mmoja.
“Tuna furaha kuanza kampeni zetu kwa ushindi kwenye juhudi za kutetea taji hilo tuliloshinda msimu uliyopita,” alisema nahodha wa KU.
Aliongeza kuwa ana imani tosha wataendeleza mtindo wa kushinda kwenye mechi zijazo.
Hata hivyo alipongeza mnyakaji wao Sharon Emali kwa kuibuka mchezaji bora wa mechi hiyo. Mlinda lango huyo alisaidia pakubwa kwa kuokoa shuti nyingi tu za wapinzani langoni.
Nayo Phoenix ilionyesha inalenga kubeba taji la msimu huu kwa kuzoa ushindi mnono. Wafungaji walikuwa James Mwangi aliyetikisa wavu mara nne.
Nao Shadrack Kaval, Japheth Mayibe, Abel Moses, Hermaton Gicheru na Bonface Mayaka kila mmoja alifunga bao moja.
“Ninapongeza wachezaji wangu kwa kuonesha kazi nzuri kwenye utangulizi wa mechi za msimu mpya,” alisema kocha Phoenix iliyomaliza ya pili muhula uliyopita.
Aliongeza kuwa licha ya hayo wanafahamu wapinzani wamepanga kuwavuruga ligini.