MAONI: Mchujo wa Kasipul umemweka Naibu Gavana Magwanga pabaya katika ODM
MCHUJO wa ODM katika eneobunge la Kasipul umemchongea Naibu Gavana Oyugi Magwanga na kuiacha Kaunti ya Homa Bay kama imegawanyika zaidi kisiasa.
Homa Bay imekuwa kati ya kaunti ambazo zinasifika kutokana na miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya kitaifa.
Rais William Ruto amezuru kaunti hiyo mara nyingi zaidi kuliko yoyote ile nchini huku akizindua miradi mbalimbali ya maendeleo, baadhi ambayo imekamilika na mingine bado inaendelea.
Hata hivyo, kumekuwa na gumzo na lawama kuwa utawala wa Kaunti haufanyi chochote na unajivumisha kwa kutumia miradi ya serikali ya kitaifa.
Mwanzo, mchujo wa ODM umeanika uhasama wa kichinichini ambao umekuwepo kati ya Gavana Gladys Wanga na naibu wake Oyugi Magwanga.
Wakati wa kampeni za kuelekea mchujo huo, ilikuwa wazi kwamba Bi Wanga na wabunge wa ODM walikuwa wakiunga mkono Boyd Were, mwanawe marehemu Mbunge Ong’ondo Were.
Kwa upande mwingine, Bw Magwanga alikuwa kimya wakati wa kampeni za mchujo huo japo duru zilikuwa zikiarifu alikuwa akimuunga mkono Newton Ogada ashinde tikiti hiyo.
Ziliposalia siku tatu kabla ya mchujo, Bw Magwanga aliandaa mkutano wa umma ambao alikemea sana chama cha ODM na kusema hangekubali Kasipul walazimishiwe viongozi.
Naibu huyo wa gavana ambaye anatoka Kasipul alisema wakazi wa eneo lake wanahitaji kiongozi ambaye ana maono ya kuendeleza miradi ya maendeleo wala si wa kuendeleza matakwa yao viongozi wa ODM.
Kauli ya Bw Magwanga ilimwekea pabaya na viongozi wengine wa ODM ambao walimtaja kama msaliti asiyethamini chama.
Baadhi hata sasa wanapendekeza atengwe kwenye uongozi wa kaunti, wengine wakitaka abanduliwe kama naibu gavana.
Mnamo 2022, Bw Magwanga alikuwa akisaka ugavana lakini akashawishiwa na uongozi wa ODM amuunge Bi Wanga kisha naye akapewa unaibu gavana.
Kwenye kura ya 2017 aliwania ugavana dhidi ya Cyprian Awiti lakini akabwagwa, akawasilisha kesi mahakamani ambayo ilishia Mahakama ya Juu lakini akashindwa.
Wakati alipokuwa mbunge Bw Magwanga alikuwa kati ya wabunge wachapakazi nchini na huenda siasa zake bado zinasukumwa na ari ya kutaka ugavana 2027.
Hata hivyo, hatua yake ya kuenda kinyume na ODM itamponza kwa sababu siasa za Homa Bay nazo zina miegemeo ya chama.
Iwapo Bi Wanga na Bw Magwanga hawataridhiana, basi hii itakuwa mwanzo wa siasa kali za miegemeo Homa Bay.
Aidha mchujo wa ODM pia umechemsha kaunti ikizingatiwa Bw Ogada hajakubali kushindwa na amewasilisha malalamishi yake kwenye jopo la kutatua mizozo ya ODM.
Ghasia ambazo zilitokea Kasipul zimewaacha wengi na makovu na maswali ya jinsi ambavyo kampeni za 2027 zitakavyokuwa.
Hii ni kwa sababu kaunti hiyo imekuwa kitovu cha ghasia za kisiasa miaka ya nyuma hasa wakati wa michujo inayoandaliwa katika kila uchaguzi.
Aidha wawaniaji mbalimbali kando na ODM wamefanya siasa ya Kasipul ionekane kama iliyojaa chuki na demokrasia inakandamizwa.
Baadhi ya wawaniaji hasa wamekuwa wakilenga familia ya marehemu mbunge Ong’ondo Were na kutumia maovu wakati wa utawala wake kuwapiga vita kisiasa.
Ni vyema iwapo kila mwaniaji atakuwa akieneza sera zake kwa njia ya amani kisha raia waachiwe jukumu la kuamua mshindi badala ya hii siasa ya kupakana tope.