Habari za Kitaifa

Besigye ashtaki mawaziri wa Kenya kwa tukio la kutekwa nyara akiwa Nairobi

Na SAM KIPLAGAT September 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KIONGOZI wa upinzani nchini Uganda, Dkt Kizza Besigye, anataka Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen na mwenzao wa Ulinzi Soipan Tuya, watangazwe kuwa hawafai kushikilia nyadhifa za umma kutokana na kutekwa nyara kwake akiwa Kenya na kupelekwa Uganda kushtakiwa.

Besigye, 68 na msaidizi wake wa kisiasa, Obeid Lutale, wanasema katika kesi waliyowasilisha katika Mahakama Kuu kuwa maafisa hao wakuu wa serikali wanawajibika pamoja kwa ukiukaji wa katiba, kuhusiana na kutekwa nyara kwao na kupelekwa Uganda mnamo Novemba 16, 2024.

Wanasema kwamba kutekwa nyara kwao na kuondolewa Kenya kulifanywa na polisi kutoka Uganda kwa kushirikiana na vikosi vya usalama vya Kenya bila kufuata taratibu zozote za kisheria.

Kesi hiyo inasema serikali ya Uganda imethibitisha kuwa kutekwa nyara kwao kulifanywa kwa kushirikiana na maafisa wa serikali ya Kenya.

“Amri itolewe kwamba washtakiwa walikiuka Katiba hivyo basi hawafai kuwa madarakani chini ya Katiba hii,” wanasema katika kesi yao jijini Nairobi.

Maafisa wengine waliotajwa kama washtakiwa ni Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Uhamiaji Evelyn Cheluget, na Afisa Mkuu wa Uhamiaji katika Kituo cha mpakani cha Malaba.

Kesi ilipofikishwa mbele ya Jaji Lawrence Mugambi jana, Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor aliomba muda zaidi kuwasilisha majibu yake.

Lakini wakili mkuu Martha Karua na James wa Njeri walisema kuwa stakabadhi za kesi ziliwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu Julai 28.

Jaji Mugambi alitoa siku 14 kwa Bi Oduor kuwasilisha majibu na akapanga kesi kuanza kusikilizwa Februari 25.

Mbali na kutaka maafisa hao watangazwe hawafai kushikilia nyadhifa za umma, Dkt Besigye anataka pia alipwe fidia kwa kukamatwa kupitia mbinu haramu.

“Iamuliwe kwamba kuhamishwa na/au kurejeshwa kwa walalamishi kutoka Kenya hadi Uganda kulikuwa haramu, hakukuzingatia Katiba na hakukufikia vigezo vya Sheria ya Uhamiji (Nchi za Jumuiya ya Madola) Kifungu 77,” wanasema katika kesi yao.

Wawili hao walikamatwa Novemba 16 2024 jijini Nairobi baada ya kualikwa kwa uzinduzi wa kitabu cha Bi Karua.

Walisema kitendo cha kuruhusu maafisa wa usalama wa nchi nyingine kuendesha operesheni ndani ya mipaka ya Kenya ni ukiukaji wa majukumu na kusaliti katiba.

Wanasema kuwa, ukweli kwamba hatua hiyo ilifanywa kwa kushirikiana na Uganda ni dalili ya wazi kwamba maafisa wa serikali walikiuka uhuru na mipaka ya Kenya, na kusababisha uharibifu mkubwa wa usalama wa taifa kwa kuruhusu maafisa wa usalama wa nchi nyingine kufanya operesheni ndani ya mipaka ya Kenya.

“Hili peke yake linaonyesha kuwa washtakiwa hawafai kushikilia madaraka na kutumia mamlaka ya umma kwa kukiuka Kifungu cha 1 cha Katiba, kinachosema “Mamlaka yote makuu ni ya watu wa Kenya na lazima yakelezwe tu kwa mujibu wa Katiba hii,” wanasema.

Viongozi hao wawili walisema dakika chache kabla ya kutekwa nyara, wanaume wapatao wanane waliovaa kiraia na kujihami kwa bastola walijiwasilisha kwao kama maafisa wa Polisi wa Kenya na kuwaambia wanakamatwa. Walipelekwa chumba cha chini cha jengo walilokuwa.

Baadaye walisombwa kwenye gari moja pamoja na watu wanne wakiwemo dereva, huku watu wengine watatu wakiwa katika magari mengine matatu.

Magari hayo mengine matatu yaliwafuata hadi kituo cha mafuta ambako gari lao lilijazwa mafuta na kisha wakaelekea moja kwa moja hadi Kituo cha mpakani cha Malaba.

“Na ndipo tulijua kuwa watu wanne waliokuwemo kwenye gari walikuwa Waganda baada ya kuwasikia wakiongea katika lahaja ya Ankole,” Dkt Besigye alisema.

Walipofika Kampala, wawili hao walizuiliwa bila mawasiliano katika Kambi ya Wanajeshi ya Makindye.

Dkt Besigye na msaidizi wake walifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi iliyoko Makindye, Uganda wakishtakiwa kwa kosa la kuwa na silaha wakiwa Kenya, kinyume cha Sehemu ya 1 na 2 ya Sheria ya Silaha ya Uganda.

Wanawakosoa maafisa wakuu wa serikali kwa kuwezesha kukamatwa kwao na kurejeshwa Uganda, jambo ambalo limewafanya kudhulumiwa kisiasa, kushtakiwa, kudharauliwa, kunyanyaswa na kukabiliwa na vitisho vya maisha yao.

Walisema licha ya kukamatwa ndani ya ardhi ya Kenya, hawakufikishwa mahakamani ndani ya muda uliowekwa katika Kifungu cha 49(1)(f) cha Katiba.

“Badala yake, walikabidhiwa maafisa kutoka Jamhuri ya Uganda, hatua ambayo haikutegemea au kuidhinishwa na Katiba au sheria yoyote ya Kenya,” wanaeleza katika kesi yao.