Mvulana ‘alivyookoa’ babaye mgonjwa kupitia TikTok
VINCENT Kaluma, mvulana wa miaka 18 kutoka kijiji cha Ngaru, Othaya, Kaunti ya Nyeri, ametikisa taifa baada ya kutumia TikTok kuonyesha maisha yake ya kila siku akimhudumia babake mgonjwa.
Video zake, zilizomuonyesha akichanganya kazi ya shamba na kumtunza babake aliyepooza baada ya kupatwa na kiharusi, ziligusa mioyo ya maelfu.
Awali, Kaluma alikuwa akichapisha video za ucheshi, lakini alipoamua kuonyesha hali halisi nyumbani, aliguswa na jumbe za faraja na usaidizi kutoka kwa wafuasi wake.
Watu wengi walimtia moyo kuendelea kuelezea safari yake, wakitumaini kuwa wema wa watu ungemfikia.
Hatimaye, mnamo Septemba 28, kijiji chao kiligeuka kuwa uwanja wa upendo. Mamia ya watu waliovutiwa na hadithi yake walifika kumpa msaada.
Waliwasili kwa pikipiki, matatu na magari binafsi wakiwa wamebeba vyakula, unga, samani, simiti na hata pesa taslimu.
Madaktari waliokuwepo walijitolea kumtibu babake, huku kampuni kadhaa zikimpa kazi ya kuwa balozi wa kuvumisha bidhaa.
Kaluma, anayetamani kusomea uuguzi, alisema kulea babake kumempa moyo wa kutaka kuwahudumia wagonjwa.
“Napenda uuguzi kwa sababu nimeutumia nyumbani. Kumtunza babangu ndiko kumenipa msukumo,” alisema.
Tukio hilo lililojulikana kama “Kaluma Day” lilifanyika bila wanasiasa kupewa nafasi ya kuzungumza. WanaTikTok waliamua iwe ni siku ya matumaini, mshikamano na heshima kwa kijana huyo mkweli.
Mchango huo ulipatia familia ya Kaluma matumaini mapya. Mama yake, Bi Beatrice Wangechi, alisema kwamba hajawahi kuona mshikamano wa aina hiyo maishani mwake.
“Nilikuwa nikiomba misaada ya karo na matibabu, lakini safari hii watu walikuja wenyewe na kwa moyo wa hiari,” alisema kwa mshangao.
Kaluma alipata ahadi ya kusaidiwa kuendelea na elimu, huku kampuni mbalimbali zikiahidi kumfadhili kusomea uuguzi.
Hadithi ya Kaluma ni ya maumivu, matumaini, na ushindi wa utu kupitia mitandao ya kijamii.