Polisi 5 washtakiwa kuiba na kuuza bunduki; wadaiwa kupatwa wakiwa na risasi 1,000
MAAFISA watano wa polisi na askari mmoja wa magereza wanaoshukiwa kuhusika katika uuzaji haramu wa bunduki na risasi, watajua leo Jumanne ikiwa watazuiliwa kwa wiki mbili zaidi huku uchunguzi wa kesi yao ukiendelea.
Maafisa hao sita walikamatwa wakidaiwa kuwa na zaidi ya risasi 1,000 ambazo zinashukiwa kuwa zilikusudiwa kuuzwa nchini Sudan.
Hakimu Mkuu wa Milimani, Lucas Onyina, alisema atatoa uamuzi wake Septemba 30 kuhusu ombi la Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) la kutaka kuendelea kuwazuilia washukiwa hao kwa muda wa siku 14 ili kukamilisha uchunguzi.
DCI iliomba mahakama iwaruhusu kuwazuilia maafisa hao kwa siku 14 ikisema kuwa suala hilo ni la usalama mkubwa wa taifa na lina maslahi ya kitaifa.
Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ilisema kuwa maafisa hao wanashukiwa kusafirisha silaha na risasi hadi mji ulio mpakani mwa Kenya na Sudan Kusini, eneo ambalo limekumbwa na mizozo ya mara kwa mara ya mipakani.
Washukiwa hao wanachunguzwa kwa makosa ya kumiliki mali ya serikali kinyume cha sheria, kula njama kutenda kosa la jinai, na kumiliki bunduki na risasi bila vyeti halali.
Maafisa waliofikishwa mahakamani Milimani ni Isaac Kipngetich, Cyrus Kisamwa, Samson Mureithi Mutongu, Wesley Sang, Paul Kipketer Tonui na askari wa magereza Charles Lotira Ekidor.
Katika ombi la DCI, mahakama iliombwa iwaruhusu kuwazuilia washukiwa katika kituo cha polisi cha Capitol Hill huku uchunguzi ukiendelea.
Mahakama iliambiwa kuwa polisi wanahitaji kufanya uchunguzi wa bunduki na risasi hizo.
“Hili ni suala la maslahi makubwa ya umma, hivyo naomba mahakama hii iwaruhusu polisi kuendelea kuwazuilia washukiwa kwa siku 14,” alisema mwendesha mashtaka.
Afisa wa DCI, Bw Hillary Kimuyu, alisema taarifa za kijasusi zinaonyesha kuwa maafisa hao sita wamehusika katika biashara haramu ya silaha.
Bw Kimuyu alisema washukiwa walikamatwa jijini Nairobi na mjini Eldoret ambapo walipatikana na bastola ya aina ya Remington Rand Model na sehemu za kuhifadhi risasi 19.
Aliongeza kuwa Kisamwa na Mutongu walihusika katika kusafirisha risasi kutoka ghala la serikali jijini Nairobi ambako wameajiriwa.
Ekidor, askari wa magereza, alitarajiwa kupokea risasi hizo na kuzisafirisha hadi Lodwar.
“Ripoti za kijasusi zinaonyesha kuwa Ekidor anahusishwa na uuzaji wa risasi katika soko la Lokichogio, karibu na mpaka wa Kenya na Sudan Kusini. Sang ndiye mhifadhi wa funguo za ghala ambako bunduki hizo zimehifadhiwa,” Bw Kimuyu alifichua.
Afisa huyo wa DCI aliongeza kuwa kuna hofu kuwa maafisa hao wanaweza kuingilia uchunguzi kwa kuwasiliana na raia au maafisa wa ngazi za chini.
Aidha alisema washukiwa wanaweza kuficha ushahidi ambao bado haujapatikana.
“Tunapanga kufanya uchunguzi wa balistiki, uchunguzi wa kidijitali na wa mitandao, pamoja na kuwakamata washukiwa wengine walioko Turkana na Nairobi,” alisema.
Kukamatwa kwa maafisa hao kunajiri wiki tatu tu baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kufichua kuwa kuna silaha zinazoibwa kutoka maghala ya serikali na kuuzwa kwa majambazi na maafisa wa polisi walioko maeneo yenye mizozo kama vile North Rift.