Makala

Mshtuko, majonzi ikibainika walioangamia ajalini Kariandusi ni 16 wa familia moja

Na MWANGI MUIRURI September 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

FAMILIA moja katika eneo la Kandara, Kaunti ya Murang’a, ilifahamu kupitia vyombo vya habari kuhusu ajali mbaya ya barabarani iliyotokea Kariandusi katika Barabara ya Nakuru-Nairobi, zaidi ya kilomita 200 kutoka nyumbani.

Mnamo Septemba 28, 2025, taarifa ya habari ilieleza kuwa watu 13 walifariki baada ya matatu ya viti 14 kugongana na trela.

“Nilipokuwa nimekaa chini ya mti kijijini Kahiga nikisikiliza redio, habari hiyo ilinifanya nihisi baridi kali mwilini na kizunguzungu. Kwa namna fulani nilihisi ajali hiyo ilihusiana na familia yangu. Nilijikuta nimechanganyikiwa na nikaondoka,” asema Bw Charles Maina, mwenye umri wa miaka 54, ambaye ndiye msemaji wa familia.

Anakumbuka jinsi taarifa hiyo ilivyosema:

“Ripoti za awali zinaonyesha kuwa matatu ilikuwa inakimbia kupita kiasi na ilipokuwa ikijaribu kupita gari jingine ndipo iligongana na trela. Wakazi walijitokeza kusaidia manusura huku polisi na vikosi vya uokoaji wakifanya kazi ya kuwaokoa waliokwama na kuwatambua waliopoteza maisha.”

Maina anaeleza kuwa asubuhi hiyo saa kumi alfajiri, watu 13 wazima wa familia pamoja na watoto watatu walikuwa wameabiri matatu hiyo kwenda Gilgil kumtembelea ndugu yao Pauline Muthoni (65), aliyekuwa mgonjwa.

Dereva wa matatu hiyo alikuwa kijana wa familia mwenye umri wa miaka 28, Bw Elijah Mburu, ambaye pia alifariki katika ajali hiyo.

Alieleza kuwa Bw Mburu alifika kijijini Kandara saa tatu usiku na kuanza safari hiyo baada ya kupumzika kwa muda wa saa tatu tu.

SOMA PIA: Watu 13 wafariki katika ajali matatu ilipogongana na trela Gilgil

Mamake Mburu, mwenye miaka 65, alikataa kujiunga na safari hiyo dakika za mwisho, jambo lililomwokoa. Hata hivyo, alipoteza mwanawe, wazazi wake wote wawili, na dada zake wanne.

“Sitaki kuzungumza kuhusu hili. Niko hai kwa sababu ya upendo wa Mungu. Nimehuzunika sana, lakini namwachia Mungu anayejua maana ya yote haya,” alisema mama huyo, ambaye sasa ndiye dada pekee aliye hai kati ya ndugu 12 wa familia hiyo.

Bw Maina alisema familia hiyo inajulikana sana kama “Ya Gicheru wa Gatari”, ikiwa na makazi katika vijiji vya Kahiga, Kangui na Gacharage.

“Nilikaa chooni kwa takriban saa moja nikiwa na maumivu ya tumbo lakini hakuna kilichotokea, niliamua kutoka na kukabiliana na ukweli,” asema.

Alipokutana na ndugu wengine, walikuwa wameanza mkutano usio rasmi, kila mmoja akiwa na wasiwasi lakini bila habari kamili.

“Ilipofika saa saba mchana, simu zilikuwa zimefurika za kuthibitisha kile tulichokuwa tukihofia: kwamba ajali hiyo ilikuwa imewapata wapendwa wetu,” asema Maina.

Wengine walibaki na matumaini, wakisisitiza wasubiri taarifa rasmi kutoka kwa waliokuwa safarini. Simu ziliendelea kupigwa bila mafanikio – hali hiyo ya kimya ilizidi kuwa thibitisho la baya zaidi.

“Tulianza kuhesabu, kama watu 13 wakubwa na watoto watatu walikuwa kwenye gari hilo, nani basi aliyenusurika?” alihoji Maina. Saa moja baadaye, taarifa ya pili ya habari ilisema vifo viliongezeka hadi watu 14.

“Nyumba yetu iligeuka uwanja wa maombolezo. Kilio, vilio, na mbio za kupoteza fahamu. Majirani walianza kuwasili, na kufikia jioni, makazi yetu yalikuwa kama makaburi,” alisema.

Nduguye Maina, Bw Zachariah Mwangi (45), alisema kufikia saa tatu usiku, familia ilikuwa imejawa na hisia nyingi, kila mmoja akielezea huzuni kwa njia yake.

“Wengine walikuwa wamelala kifudifudi wakipiga kelele, wengine wakiomba kwa ndimi, wengine wakilia kwa nguvu, wengine wakitaka kujitoa uhai. Majirani walilazimika kuwashikilia chini au kuwafunga kwenye miti,” alisema Mwangi.

Aliongeza: “Familia yangu ilipoteza watu sita: baba yangu Elijah Mburu Kiboi (85), mama yangu Lydiah Njeri (75), mapacha Naomi Wangui na Joyce Wambui (35), dada yangu Catherine Njambi (30), na Pauline Muthoni (28).”

Jana, orodha rasmi ilithibitisha kuwa wote 16 waliokuwa ndani ya gari hilo walikuwa wamefariki.

Katika makazi ya Kangui, Bw Robinson Karanja (85), kaka wa Lydiah Njeri, pia alikufa. Binti zake wawili – Naomi Wangui (28) na Beatrice Waithera (34), walifariki pamoja na mtoto wa Beatrice aitwaye Wanjiru.

Katika makazi ya Gacharage, Grace Waithera (65) alifariki pamoja na binti yake Judy Ruguru.

Afisa Mkuu wa Afya wa Kaunti ya Murang’a, Bw Eliud Maina, alisema wanapanga kutuma washauri wa kisaikolojia kusaidia familia hiyo.

“Wanahitaji usaidizi wa kitaalamu ili kupona. Gavana Irungu Kang’ata atazuru familia na kupeleka timu ya washauri kusaidia kupona,” alisema Maina.

Hata hivyo, familia hiyo inalalamika kuwa hali yao ya kifedha haiwezi kuwasaidia kulipia gharama inayotajwa.

“Tunaambiwa bili za hospitali, kuhifadhi miili na huduma za dharura zinafikia Sh1.5 milioni. Uchunguzi wa miili ni Sh300,000. Gharama za mazishi bado hazijahesabiwa. Hii ni bajeti ya zaidi ya Sh3.5 milioni. Tutazipata wapi?” alihoji Bw Boniface Njaramba.

Familia hiyo imeomba wahisani kuingilia kati kusaidia kugharamia bili na mazishi ya wapendwa wao wote 16 waliofariki.