Habari za Kitaifa

Kilimo na riadha kuuzwa kama vivutio vya watalii nchini Kenya

Na MISHI GONGO September 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI imesema kuwa inapanga kuongeza utalii wa kilimo na michezo ili kuwavutia watalii zaidi nchini.

Akiongea Jumanne, Septemba 30 katika kongamano la washikadau wa utalii mjini Mombasa, waziri wa utalii Rebecca Miano, alisema Kenya inapania kuongeza bidhaa zaidi za kuuzia watalii ili kufikia azma yake ya kufikia watalii milioni 5.5 kufikia mwaka 2027.

Waziri wa Utalii Bi Miano alisema kuwa watalii wengi wanavutiwa na urithi wa kilimo cha Kenya pamoja na uwezo wa nchi kuwakuza wanariadha mashuhuri duniani.

“Kuna watalii wanaotaka kujionea mahali kahawa na chai zinakopandwa hadi kufika kikombeni. Wengine wanataka kufahamu ni kwa nini Kenya huzalisha mabingwa wa riadha. Tunataka kufungasha fursa hizi na kuonyesha utamaduni wetu, urithi na mashujaa wetu,” akasema Bi Miano.

Kongamano hilo pia lililenga kuboresha uchumi wa Pwani kufuatia kuboresha miundo msingi ya sehemu za kitalii kama mbuga za wanyama na majumba ya kihistoria kama Fort Jesus.

Bi Miano alisema Pwani ndiyo uti wa mgongo wa utalii nchini, lakini akasisitiza haja ya uwekezaji upya ili kuendeleza mvuto wake na kuhimili ushindani wa kanda ya Afrika Mashariki.

“Tuko katika hatua ambapo tunapaswa kukarabati hoteli na vifaa vilivyopo na pia kuvutia ushirikiano na uwekezaji mpya utakaoinua Pwani kufikia viwango vipya tunavyotaka,” akaeleza.

Serikali inalenga kufikisha wageni milioni 5.5 ifikapo mwaka 2027, kupitia kuongeza ndege za moja kwa moja kutoka mataifa mbalimbali na urahisi wa kupata viza.

Kwa sasa mashirika ya ndege ya kimataifa yakiwemo Fly Dubai, Turkish Airlines na Air Asia pamoja na ndege za kukodi huwasili katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta na ule wa Moi Mombasa

“Tunaendelea na mazungumzo na karibuni huenda tukaona mashirika zaidi yakipewa nafasi kuingia nchini. Kufungua anga ni jambo muhimu ili kuongeza upatikanaji wa huduma na ushindani wa vivutio vyetu,” akasema Waziri.

Naibu Gavana wa Kilifi Bi Flora Mbetsa ambaye pia alihudhuria kikao hicho, alisema msukumo huu mpya utafungua nafasi nyingi za ajira kwa vijana wa Pwani.

“Kama Pwani tunazo bidhaa nyingi za kuvutia wageni. Tukipata uangalizi wa serikali, tunatarajia fursa zaidi na tunawahimiza vijana kujitosa katika taaluma ya utalii,” akasema.

Utalii ni mojawapo ya sekta kuu zinazoliingizia taifa mapato ya kigeni. Bi Miano alisema serikali inapania kutumia vivutio vya kipekee vya Pwani, kuboresha miundomsingi na kupanua ushirikiano ili kuhakikisha sekta ya utalii inaendelea kuchangia pakubwa katika uchumi wa nchi.

“Tunacho cha kutosha cha kutoa, na huu ndio wakati wa kuifanya Pwani kuwa eneo tofauti na lenye mvuto zaidi kitalii, si tu Afrika Mashariki bali pia kimataifa,” akasema Waziri.