Zogo la Uhuru, Gachagua kupigania usemaji wa Mlima lahatarisha umoja wa Upinzani
MZOZO wa kisiasa unaotokota kati ya Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua unaweka hatarini juhudi za kubuni muungano wa upinzani nchini kila mmoja akijisawiri kama msemaji wa eneo la Mlima Kenya.
Mgogoro unaoendelea unaonyesha nyufa ambazo wachambuzi wanasema zinaweza kudhoofisha umoja wa upinzani dhidi ya Rais William Ruto.
Naibu Kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), Cleophas Malala, amekashifu chama cha Jubilee kinachoongozwa na Uhuru akidai kina njama ya kuhujumu DCP na kudhoofisha umaarufu wa Gachagua.
Malala anadai kwamba, Jubilee inashirikiana na UDA ya Rais Ruto chini ya maji kugawanya Mlima Kenya, eneo ambalo Gachagua amekuwa akijijengea umaarufu tangu alipoondolewa serikalini.
“Sitoki eneo la Mlima Kenya; hivyo naweza kuzungumza na jioni kurudi Kakamega kula ugali wangu. Chama hicho (Jubilee) kinapaswa kuonywa kisije kikasababisha mgawanyiko, ikiwa kweli ni sehemu ya Muungano wa Upinzani,” alisema Malala.
Alisema kwamba Jubilee inaonekana kuungana na UDA ya Dkt Ruto, akikifananisha na wilibaro nyekundu ndani ya Mt Kenya.
“Ukifanya kazi na Kasongo (Ruto) na umetumwa na wilibaro nyekundu haumtakii mema kiongozi wetu na DCP kwa ujumla,” alisema Malala.
Hii ni baada ya Jubilee kupitia Katibu Mkuu wake Jeremiah Kioni kumkashifu Gachagua kwa kujaribu kumtaka Dkt Fred Matiang’i kuunda chama chake badala ya kujiunga na Jubilee.
Kioni alisema Gachagua alimtaka Matiang’i apuuze Jubilee na kujiunga na chama kidogo chenye mizizi kutoka eneo la Kisii.
“Yeye ni mradi wa Rais Ruto na anajaribu kudanganya Wakenya,” alisema Kioni kuhusu Gachagua kwenye mahojiano Jumanne.
Lakini mchambuzi wa siasa, Prof Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multi Media, anatoa tahadhari kuwa vita vya maneno kati ya Jubilee na DCP vinaweza kuua muungano wa upinzani kabla hata ya uchaguzi wa 2027.
Alisema kambi ya Uhuru ina hofu kutokana na kudidimia kwa ushawishi wake Mlima Kenya na ndio maana inapiga kelele bila kuzingatia madhara ya kufanya hivyo.
“Wanataka Matiang’i aungwe mkono Mlima Kenya. Sasa wanatafuta njia ya kuvunja muungano,” alisema Prof Naituli.
Prof Naituli pia alipuuza madai kwamba Gachagua ndiye anayevuruga umoja wa upinzani.
“Ikiwa kuna anayependa Ruto arejee Ikulu, ni Uhuru mwenyewe. Tuliona jinsi alisaidia Raila 2022—akampigia kampeni kabisa. Kudai kuwa Gachagua ni mradi wa Ruto kunaonekana kuwa utani,” alisisitiza.
Muungano wa upinzani unaonekana kuwa tete zaidi baada ya Uhuru kufufua Jubilee, na matukio ya hivi punde yameonyesha wazi vita kati yake na Gachagua.
Mbunge wa Embakasi Kaskazini, James Gakuya, ambaye ni mshirika wa Gachagua, anasema Jubilee inaonekana imechagua kusimama peke yake katika uchaguzi wa 2027:
“Kulikuwa na wazo kwamba, upinzani utakuwa mmoja, ambapo Jubilee ingekuwa sehemu yake. Lakini kwenye mkutano wa Jubilee wa juzi, inaonekana wameamua kwenda peke yao, labda kuunga mkono mgombea wao ambaye huenda ni Matiang’i,” alisema Gakuya.
“Sijali kabisa kwa sababu Matiang’i atavutia tu kura za Kisii. Nina uhakika kwamba, kura za Mlima hazitagawanyika kwa sababu Uhuru Kenyatta amechagua mgombea mwingine.”
Mbunge wa Githunguri, Gathoni Wamuchomba, wa mrengo wa Kenya Moja, alisisitiza kwamba Uhuru bado ndiye msemaji wa Mlima Kenya.
“Aliunganisha nchi. Sasa ana uhuru wa kumchagua yule atakayeendeleza kazi yake,” alisema Wamuchomba.
Alionya dhidi ya siasa za kuhukumu akisema hakuna chama au mwanasiasa anayeweza kudai ana ushawishi wa kura za Mlima.
“Ni huzuni kuona watu wa Mlima wakipigana kwa sababu ya siasa; haki hii ya kujiamini imezidi! Kabla ya DCP, kulikuwa na Jubilee, UDA, DP na wengine. Hakuna aliyekuwa na haki ya kura milioni nane za Mlima. Tulisema zamani hatupangwingwi! Uhuru Kenyatta ndiye kinara wa Mlima,” aliongeza.
Wachambuzi wanaonya kwamba mzozo huu unaweza kusababisha upinzani kugawanyika zaidi wakati ambapo umoja unahitajika zaidi kupinga utawala wa UDA wa Rais Ruto. Prof Naituli asema, Jubilee na DCP zinapaswa kuacha lawama na badala yake zisukume ajenda zao za kisiasa.