Sababu za IEBC kunasa mboni za macho za wanaojisajili kupiga kura
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeanzisha teknolojia mpya ya usajili wa wapiga kura inayojumuisha kunasa mboni za macho kwa mara ya kwanza, huku ikilenga vijana wa kizazi cha Gen Z wanaotarajiwa kuwa na ushawishi mkubwa katika uchaguzi wa 2027.
Katika juhudi za kuwalenga vijana waliotimiza umri wa miaka 18 kujisajili kama wapiga kura, IEBC imepanua maeneo ya usajili hadi Vituo vya Huduma kote nchini, pamoja na kupeleka vifaa vya usajili katika ofisi zote za maeneobunge 290.
Kwa mujibu wa kamishna wa IEBC Bi Anne Nderitu, vifaa hivyo vipya vya kidijitali vinavyotumia mfumo wa Electronic Voter Identification System (EVID) vina uwezo wa kunasa alama za vidole na mboni za macho, tofauti na vifaa vya zamani vya BVR vilivyokuwa vikubwa na vya kusumbua.
“Sasa tunatumia tableti ndogo, zenye uwezo mkubwa wa kuchukua taarifa sahihi za mpiga kura kwa usalama wa hali ya juu,” alisema Bi Nderitu katika mahojiano ya moja kwa moja kupitia kipindi cha Fixing the Nation cha runinga ya NTV.
IEBC pia imepanga kuanzisha fomu za usajili wa awali, zitakazowezesha vijana kuanza mchakato wakiwa nyumbani na kisha kufika ofisini kuchukuliwa alama za vidole na picha.
Kulingana na takwimu za IEBC, kuna Wakenya milioni 6.3 ambao wamefikisha umri wa kupiga kura lakini hawajasajiliwa, wengi wao wakiwa ni wa kizazi cha Gen Z waliozaliwa kati ya mwishoni mwa miaka ya 1990 na 2010.
Hii ni sehemu ya mpango wa IEBC wa kufanikisha usajili wa wapiga kura wapya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027, ambao unatarajiwa kufikisha idadi ya wapiga kura kuwa milioni 28.4, baada ya kuondoa waliopoteza maisha kutoka orodha ya sasa ya wapiga kura milioni 22.1.
“Kwa sasa kijana yeyote anaweza kujisajili akiwa mbali na nyumbani na taarifa zake zionekane katika kituo anachokipendelea,” alisema Bi Nderitu, akibainisha kuwa vifaa vya usajili vinapatikana katika kila eneobunge.
IEBC pia imetangaza kuwa usajili utafanyika katika taasisi za elimu ya juu na kwa kutumia vifaa vya kuhamishwa, huku kampeni zikielekezwa kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali ili kuwavutia vijana ambao hawajasajiliwa.
Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Ethekon, amesema tume inaendesha kampeni kali ili kuhimiza vijana kujitokeza kwa wingi kujisajili.
Katika uchaguzi wa 2022, Dkt William Ruto alishinda kwa kura 7,176,141 dhidi ya Bw Raila Odinga aliyepata kura 6,942,930.
Hata hivyo, kati ya wapiga kura milioni 22.1 waliokuwa wamesajiliwa, ni milioni 14.3 pekee waliopiga kura huku takriban milioni nane wakikosa kushiriki, wengi wao wakiwa vijana.
Ripoti ya IEBC ilionyesha kuwa vijana milioni 8.8 (asilimia 40 ya wapiga kura wote) walikuwa wamejisajili kabla ya uchaguzi huo, lakini sehemu kubwa hawakujitokeza siku ya kupiga kura.
Sasa, kwa kutumia teknolojia mpya na mikakati ya kisasa, IEBC inalenga kuhakikisha vijana wanajisajili na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa 2027.