Habari za Kitaifa

Korti yarudishia Sonko mamilioni yaliyokuwa yamefungiwa kwa tuhuma za wizi

Na SAM KIPLAGAT October 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA Kuu imeamuru zaidi ya Sh30 milioni zilizokuwa zimezuiwa miaka mitano iliyopita kwa tuhuma za ulanguzi wa pesa, zirejeshwe kwa aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Mike Sonko.

Jaji Nixon Sifuna aliondoa amri iliyotolewa Februari 2020, ambayo ilikuwa imezuia pesa hizo katika akaunti 10 za benki, akisema hakukuwa na msingi wowote wa kisheria wa kuamuru fedha hizo zitwaliwe na serikali kama mapato ya uhalifu.

Jaji huyo alikemea Shirika la Kutwaa Mali (ARA) kwa kufanya uchunguzi wa juu juu, akisema uchunguzi wa aina hiyo unapaswa kuwa wa kina, usio na mapungufu na wa kuaminika, kwa kuwa matokeo yake husababisha kuwajibishwa kisheria, iwe kosa la jinai au la kiraia.

“Ushahidi ulioko kwa sasa haujatosheleza kuunga mkono madai kwamba fedha zilizolengwa na ambazo ndizo kiini cha kesi hii katika akaunti mbalimbali za mtuhumiwa, ni mapato ya uhalifu,” alisema Jaji Sifuna.

Shirika hilo liliwasilisha kesi mahakamani mwaka wa 2020 likisema lilipokea taarifa kwamba Bw Sonko alihusika katika ulanguzi wa pesa, akitumia fedha zilizodaiwa kuibwa kutoka kwa serikali ya kaunti ya Nairobi.

Bw Sonko alishtakiwa Desemba 2019 kwa makosa ya mgongano wa masilahi, ulanguzuzi wa pesa na makosa mengine.

Shirika hilo liliomba na kupata agizo la kufikia, kuchunguza na kupewa stakabadhi zinazohusiana na akaunti hizo 10, ambazo zilikuwa na fedha za Dola za Amerika na Shilingi za Kenya.

Wakati wa kuomba maagizo hayo, ARA ilidai kuwa akaunti hizo zilipokea miamala ya kifedha ya kutatanisha, ambayo inasadikiwa kuwa ni mapato ya uhalifu kutokana na ufadhili haramu, wizi na shughuli za ulanguzi wa pesa kutoka kwa serikali ya kaunti ya Nairobi.

Shirika hilo lilidai kuwa kati ya Agosti 2017 na Desemba 2019, Bw Sonko alipokea kiasi kikubwa cha pesa taslimu katika akaunti mbalimbali za benki, hali iliyoonyesha dhahiri uwepo wa ulanguzi wa pesa.