Ustadi wa Raila kupangua kila utawala nchini
KWA takriban miongo minne kinara wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Bw Raila Odinga, amebobea katika karata ya kuyumbisha marais na serikali.
Mbinu za kisiasa za kigogo huyo zimekuwa zikitatiza tawala: kutoka kupinga utawala wa ‘kimabavu’ wa Rais Daniel arap Moi, kulazimisha serikali ya muungano na Rais Mwai Kibaki mnamo 2007, kufanya maelewano na Rais Uhuru Kenyatta, na sasa handisheki yake na Rais William Ruto.
Kuanzia siku zake za kutupwa korokoroni enzi za utawala wa Moi hadi handisheki na Kenyatta mnamo 2018, Bw Odinga ameendelea kuwa bingwa katika kufanya maridhiano na serikali zilizo mamlakani na kuandika upya ramani ya siasa za Kenya kila baada ya uchaguzi.
Sasa Rais Ruto anapojitahidi kumshawishi asalie upande wake huku akikaa rada kuhusu kila hatua anayopiga, kinara huyo wa ODM naye anaendelea kutoa taswira ya kutotabirika kisiasa.
Bw Odinga amerusha kibomu tena katika anga za siasa baada ya kutangaza kuwa chama chake cha ODM hakijawahi kuacha azma ya kuwania urais kwenye uchaguzi ujao wa 2027.
Kauli hiyo inajiri wakati huu anaposhirikiana na Rais Ruto katika serikali jumuishi, hali inayoibua maswali iwapo kigogo huyo mkongwe anajiandaa kujitosa tena katika debe kuwania uongozi wa taifa.
Kwa miongo kadhaa Bw Odinga amekuwa mjuzi katika kuunda miungano ya kisiasa; anaingia serikalini, anaibadilisha kutoka ndani kabla kuondoka na kurudi kwa wafuasi wake akiwa ameimarisha umaarufu, hali inayotibua mizani ya kisiasa nchini.
Mtindo huu umemfanya kuwa mmoja wa wanasiasa wasiotabirika lakini wenye ushawishi mkubwa zaidi Kenya.
Profesa Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multi Media anasema siasa za Kenya huwa hazikosi mshangao.
“Lakini jambo moja linazidi kuwa wazi: Raila Odinga hatadumu kwa muda mrefu katika serikali ya William Ruto,” asema msomi huyo wa masula ya usimamizi na utawala wa taifa.
“Kwa kweli, kufikia katikati ya mwaka ujao muungano huu wa kimaslahi uliomvutia kiongozi wa Azimio ndani ya Kenya Kwanza huenda ukavunjika.
“Raila ni mzoefu, anaelewa mwelekeo wa siasa na anajali sana ngome yake kiasi kwamba hawezi kubaki katika serikali inayoendelea kuwa kinyume cha maslahi ya kiuchumi na kidemokrasia ya wananchi,” aeleza Prof Naituli.
Anasisitiza kuwa maisha yote ya kisiasa ya Bw Odinga yamejengwa katika misingi ya kujitambulisha na maslahi ya raia wa kawaida.
Kuanzia mapambano ya kutetea vyama vingi miaka ya 1990 hadi kampeni zake za kupigania haki za wananchi miaka ya 2000 na 2010, Prof Naituli asema kigogo huyo amejisimika kama mtetezi wa mwananchi wa kawaida dhidi ya dhuluma za watawala.
“Kaulimbiu yake ya mwanamageuzi wa kupigania raia ndio msingi wa siasa zake. Hii ndiyo inampa uungwaji mkono katika mitaa ya maskini Nairobi, Kisii, Nyamira, eneo la Magharibi na Pwani. Kuivuruga kwa kuendelea kushirikiana kwa karibu sana na serikali ya Ruto ni sawa na kujimaliza kisiasa,” anahoji.