Vyama vya kisiasa vyaweka mikakati kuvutia wanawake wapigakura
KENYA inapojiandaa kwa msimu wa kisiasa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027, vyama vya siasa vinaimarisha mikakati kuvutia kundi ambalo haviwezi kupuuza- wanawake.
Kuanzia vijijini hadi mijini, wanawake bado wako mstari wa mbele katika mipango ya kampeni za vyama vyote vikuu.
Chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA), Orange Democratic Movement (ODM), na chama cha Safina vimezindua mipango inayolenga wanawake, vikisisitiza nafasi yao muhimu katika kuamua matokeo ya uchaguzi.
Wanawake ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu Kenya na walikuwa takriban asilimia 50.9 ya wapiga kura waliosajiliwa mwaka 2022.
Wachambuzi wanasemakwa kuwa wanawake ni wengi, hakuna chama kinaweza kushinda bila kuwajali.
“Wanawake wana nguvu kuanzia mashinani. Wanawake wamekuwa uti wa mgongo wa kampeni za kisiasa wakipanga mikutano, kampeni za nyumba hadi nyumba, na kuhamasisha jamii. Hii inawafanya kuwa muhimu sana,” anasema Dismas Mokua, mchanganuzi wa siasa.
“Mara wanawake wanapounga jambo au mgombeaji, mara nyingi huonekana kuwa wapiga kura waaminifu zaidi kuliko wanaume. Vyama vinatambua kuwa msaada wa kudumu kutoka kwa wanawake unaweza kuleta wingi wa wapiga kura mara kwa mara,” akaeleza.
Watetezi wa usawa wa kijinsia wanasema wanawake si tu wanapiga kura bali pia huathiri familia na vijana katika kuchagua wagombeaji.
Wiki jana, Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki alikutana na wanawake takriban 4,500 wa mashinani mjini Embu.
“Wanawake ni injini ya jamii,” Profesa Kindiki alisema.
“Wanaendesha familia na bado wanahangaika katika biashara, kilimo, na shughuli nyingine. Wanatunza maneno yao na wanaweza kutegemewa mara wanapochagua njia ya kufuata.”
Gavana wa Embu Cecily Mbarire, Mwenyekiti wa Kitaifa wa UDA, alithibitisha hoja hiyo kwa kusema wanawake ni nguzo imara ya chama na nguvu kubwa zaidi katika uchaguzi.
“Mnaweza kutegemea usaidizi kutoka kwa wanawake. Mara wanapoamini katika jambo, wanabaki imara. Wao ni wafuasi waaminifu wa UDA, na nguvu yetu hapa inategemea wao,” alisema.
Chama cha Safina chini ya kiongozi wake mpya Jimi Wanjigi kimetambua mchango wa wanawake katika uchaguzi.
Mnamo Alhamisi, Septemba 25, Safina ilimtambulisha Florence Atieno maarufu kama Atis Dollar kama mshirikishi wa Kitaifa wa Wanawake.
“Haya ni mabadiliko makubwa,” Bw Wanjigi alisema.
“Tunamkaribisha Florence katika Safina. Kazi na ujuzi wake vinajulikana, na pamoja tutajenga taifa linalojali wanawake.”
Bw Wanjigi alizungumza kuhusu changamoto za wanawake, akiahidi mabadiliko makubwa.
“Wazazi wa Nairobi, nawaheshimu. Mama ni sauti halisi ya taifa letu. Mabadiliko ya kweli yanahitajika, na Safina inatoa hayo.”
Wakati huo huo, ODM ya Raila Odinga inaboresha ajenda yake ya wanawake. Chama kimeanzisha tawi la Young Captains ndani ya ODM Women League kulenga wanawake vijana katika vyuo na vyuo vikuu. Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna, kiongozi wa wanawake Seneta Beth Syengo, na Kiongozi wa vijana Mark Ketora.
“Mtakuwa sehemu ya muundo wa maamuzi wa ODM,” Bi Syengo aliambia wanawake vijana.
“Kuanzia leo, nyinyi ndio maajenti wa chama.”
Wachambuzi wanasema wakati huu wanawake wanapiga kura kwa kuzingatia masuala kama chakula, ajira, afya, na elimu.
Kupuuza haya kuna hatari ya kupoteza kundi muhimu, wanasema.
Mtaalamu wa siasa Profesa Gitile Naituli anasema: “Kwa muda mrefu, wanawake walitumiwa kama wahamasishaji, au kujaza umati. Lakini sasa wanataka ahadi thabiti kuhusu chakula, elimu, afya, na usalama. Ndio maana kila chama kinajitahidi kuwavutia.”
“Uchaguzi wa 2027 hautahusuj tu kabila au maeneo bali pia jinsia na kizazi. Wanawake, sasa wako katikati ya vita vya uchaguzi nchini Kenya,” anasema mwanasheria Chris Omore.