Habari

Taharuki majangili wakijenga makao karibu na shule

Na SAMMY LUTTA October 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MJI wa Kainuk ulio katika mpaka wa Kaunti za Turkana na Pokot Magharibi unaendelea kukumbwa na taharuki baada ya majangili wenye silaha kujenga kraal (makazi ya  kitamaduni ya vibanda na mifugo) karibu na Shule ya Upili ya Wasichana ya Lobokat, ambayo ilifunguliwa hivi majuzi.

Shule hiyo ya kisasa, iliyokamilika mwezi Mei kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na serikali ya Kenya kupitia Mamlaka ya Barabara Kuu (KeNHA), sasa imo katika hatari kufuatia kuongezeka kwa visa vya ukosefu wa usalama.

Kwa zaidi ya wiki tano, majangili wamekuwa wakiwatatiza wakazi wa eneo la Mto Malimalite, wakivuruga amani iliyokuwa imerejeshwa kupitia Operesheni Maliza Uhalifu, na kuathiri shughuli za kiuchumi kama vile uchimbaji wa dhahabu na changarawe, kilimo na biashara ya bodaboda.

Shambulio la kijasiri zaidi lilifanyika Jumatano iliyopita ambapo Elpan Pachu, polisi wa akiba wa pekee katika kijiji cha Kailoseget, na Isaac Ilikwel, mpakiaji wa mchanga, walipigwa risasi na kuuawa mita chache tu kutoka Kituo cha Polisi cha Kainuk.

Majangili hao walitoroka na bunduki ya polisi huyo wa akiba.

“Inavunja moyo kuona haya yakifanyika karibu kabisa na kituo cha polisi,” alisema Margaret Ajikon, mkazi wa eneo hilo, akiashiria kuwa sasa ukosefu wa usalama umeanza kushuhudiwa shuleni na katika nyumba za watu.

Licha ya uwepo mkubwa wa maafisa wa usalama katika Kainuk, hakuna mtu yeyote aliyekamatwa. Wakazi wanawalaumu baadhi ya maafisa wakuu wa usalama kwa uzembe.

Bunduki ya polisi wa akiba aliyeuawa haijapatikana kufikia sasa.

“Hali hii sasa inatishia si tu usalama wa jamii, bali pia mazingira shuleni,” aliongeza Bi Ajikon.

Gavana wa Turkana Jeremiah Lomorukai, ametoa wito uchunguzi ufanywe kuhusu madai ya ushirikiano wa baadhi ya maafisa wakuu wa usalama na majangili, akiwalaumu kwa kuvuruga juhudi za miaka mingi za kuleta amani kati ya jamii za Turkana na Pokot.

“Tunahisi kuwa baadhi ya maafisa wakuu wa usalama wanajihusisha na shughuli zisizo halali mpakani badala ya kushughulikia usalama wa eneo hili,” alisema gavana huyo.

“Hatuoni tena oparesheni maalum wala majibu ya haraka kwa mashambulizi. Tunahitaji mabadiliko kamili ya mfumo wa usalama,” alisisitiza.

Alikumbusha kuwa wakati Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki alipokuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, alitangaza Hifadhi ya Kitaifa ya Turkana Kusini kuwa eneo lililopigwa marufuku kuishi watu, ili kupunguza visa vya ukosefu wa usalama.

“Hata hivyo, majambazi bado wanazurura katika hifadhi hiyo, na sasa wameanzisha kraal karibu na shule ya wasichana. Tunahitaji maafisa wa usalama wanaotekeleza majukumu yao bila kushawishiwa wala kuhongwa. Ikiwa waliopo hawawezi kuwalinda wananchi, basi waondoke,” alisema.

Ingawa Kainuk kuna vikosi vya usalama, mauaji yanaendelea.

Wakazi wameonyesha kuchoshwa na mashambulizi haya licha ya onyo kali kutoka kwa Kamati za Usalama za Kaunti za Turkana na Pokot Magharibi mnamo Agosti 28, 2025, zilizotishia kutekeleza zoezi la kuwapokonya raia silaha kwa lazima iwapo hawatazikabidhi kwa hiari.

“Tunajua kuwa mkutano wa usalama mpakani ulilenga ongezeko la silaha ndogo ndogo kama chanzo cha mashambulizi. Lakini badala ya kushughulikia majangili hao, baadhi ya maafisa wa usalama wanaonekana kuhujumu juhudi hizo,” alisema Bi Ajikon.

Alitaja hofu kuhusu ushiriki wa baadhi ya maafisa wa usalama katika uchimbaji wa dhahabu, pamoja na kuchelewa kuchukua hatua wanapoitwa kushughulikia mashambulizi.

“Kuna mtindo unaoendelea ambapo maafisa wa usalama huchukua muda mrefu sana kujibu mashambulizi, hali ambayo haikuwepo awali. Siku ya mauaji, hatua za haraka zingeweza kuzuia majanga zaidi,” aliongeza.

Bi Mary Ngilimo, mkazi mwingine, alisema majangili mara nyingi huonekana mpakani wakijifanya ni wachungaji wa mifugo karibu na shule na hospitali, pamoja na kando ya Barabara ya Kapenguria–Lokichar.

“Maficho ya majangili yanajulikana, na uwepo wao karibu na shule na barabara kuu unaonekana waziwazi. Ikiwa mamlaka haziwezi kukabiliana nao, basi zinatarajia raia wakabidhi silaha zao kwa msingi upi?” aliuliza.

Gavana Lomorukai alikubaliana na wasiwasi wa wakazi, akisema kuwa licha ya kuwepo kwa vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) katika Kituo cha Kainuk pamoja na vikosi vingine vya polisi, mashambulizi ya majangili yameongezeka.

“Takriban watu watano wameuawa mpakani, akiwemo polisi wa akiba,” alisema.

Kainuk, inayohifadhi makao makuu ya Kaunti Ndogo ya Aroo na timu ya Kamati ya Usalama ya Kaunti Ndogo, ina maafisa kutoka idara mbalimbali: Huduma ya Polisi wa Taifa, Kitengo cha Kupambana na Wizi wa Mifugo, GSU na Walinzi wa Huduma ya Wanyamapori Kenya (KWS).