Maveterani wa Tanzania walemea Kenya katika fainali Afrika Mashariki
KIKOSI cha wachezaji wa zamani wa Taifa Stars ya Tanzania kimetwaa ubingwa wa Kombe la Afrika Mashariki kwa wanasoka wa umri wa miaka 55 na zaidi.
Wanasoka hao wakongwe walitwaa taji hilo baada ya kushinda Harambee Stars ya zamani kwa bao 1-0 katika fainali bomba iliyochezwa katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN), jana.
Mshambuliaji matata mstaafu, Mohamed Hussein Daima, anayeshikilia rekodi ya ufungaji mabao 26 kwenye ligi kuu ya Tanzania, alifunga bao hilo katika kipindi cha pili baada ya kumchanganya mlinda lango wa Harambee Stars, Omar Shaban.
Kenya ilifanya mashambulizi ya mara kwa mara lakini juhudi za Mike Amwayi, Tobia Ochola, John Bobby Ogolla, John Shoto Lukoye na Sammy Omollo kuona lango la Tanzania zilizimwa na Abdi Kassim, Athnas Michael Madadi na Faza Lusozi.
Mashindano hayo ya siku mbili chini ya udhamini wa Suqoon wakishirikiana na AgeWatch yalitumiwa kuadhimisha Siku Kuu ya Kimataifa ya Watu Wakongwe ambayo husherehekewa kila Oktoba 1.

Tanzania chini ya kocha mkongwe King Abdallah Kibaden Mputa walifuzu kwa fainali hiyo baada ya kutandika Western Kenya Legends 6-1 katika nusu fainali iliyosakatwa Jumanne uwanjani humo.
Kikosi cha Kenya kinachonolewa na James Nandwa kilifuzu baada ya kushinda Uganda kwa bao 1-0.
Kila mchezaji wa vikosi vyote vinne alizawidiwa Sh12,000 na medali, mbali na vikombe vilivyopewa timu tatu za kwanza.
Daima aliibuka Mchezaji Bora wa michuano hiyo, mbali na kufunga mabao mawili.
Akizungumza wakati wa hafla ya kutoa zawadi kwa washindi, aliwapongeza mashabiki waliojitolea kwa wingi kushangilia wakongwe hao pamoja na wadhamini, huku akiwaambia kwamba wazee ndio walioweka msingi wa mambo yanayofanyika sasa.
“Kwetu Sugoon, tunapenda kusema ‘Wazee Baraka Yetu’.”
“Walifanya mengi na tumejitolea kuwakutanisha tena kupitia soka. Tumewaunganisha na vijana wa umri tofauti, wengi ambao hawakuwaona wakisakata soka miaka mingi iliyopita. Tutaendelea kuwaweka wazee wetu mbele kila wakati ili wafurahie kimwili, kiakili na kiroho.”
Aliyekuwa nyota wa timu ya taifa ya Somalia, Ahmed Sharif Ashara anayeishi Nairobi aliahidi kuandikisha timu ya zamani ya taifa hilo katika mashindano yajayo yatakofanyika Oktoba mwaka ujao nchini Tanzania.