Arsenal yalipiza kisasi dhidi ya Olympiacos ila PSG ndio dume la Barca
LONDON, Uingereza
ARSENAL walionja ushindi wao wa kwanza nyumbani dhidi ya Olympiacos katika mechi nne baada ya kuzamisha miamba wa Ugiriki 2-0 kwenye ngarambe ya Klabu Bingwa Ulaya ugani Emirates, Jumatano usiku.
Wanabunduki hao walikuwa wamepoteza 3-2 mikononi pa Olympiacos kwenye michuano ya Klabu Bingwa Ulaya (Septemba 29, 2015) na 2-1 (Februari 27, 2020) na 1-0 (Machi 18, 2021) katika Ligi ya Uropa ugani Emirates kabla ya kupata kisasi kitamu kupitia mabao ya Gabriel Martinelli na Bukayo Saka siku ya Jumatano.
Martinelli alinufaika na kazi nzito kutoka kwa mshambuliaji Viktor Gyokeres kufungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 12 kabla ya Saka kuimarisha uongozi huo katika dakika za lala-salama kutokana na asisti ya Martin Odegaard.
Hata hivyo, David Raya alifanya kazi ya ziada kupangua kombora moto kutoka kwa Daniel Podence na kuwezesha Arsenal kusalia bila kufungwa.
“Ninafurahia sana ushindi huu na kumaliza mechi bila kufungwa bao. Pongezi ziwaendee vijana wangu kwa kupata matokeo haya mazuri siku tatu tu baada ya kuchuana na Newcastle,” akasema kocha Mikel Arteta.
Mabingwa
Mabingwa watetezi Paris Saint-Germain nao walitoka chini goli moja na kulemea wenyeji Barcelona 2-1 kupitia mabao ya Senny Mayulu na Goncalo Ramos ugani Olimpic Lluis Companys.
Ferran Torres alifungia washindi wa zamani Barcelona bao la kufuta machozi katika mchuano huo wa kusisimua ambao pande zote zilionyesha juhudi kubwa katika mashambulizi.
Mpepetano kati ya Monaco na wageni wao Manchester City pia ulikuwa wa nipe-nikupe ukitamatika 2-2 na kushuhudia kadi tano za njano zikitolewa ugani Louis II.
Mvamizi matata Erling Haaland alifungia City bao la kuongoza 1-0 na 2-1 nao Jordan Teze na Muingereza Eric Dier wakasawazisha 1-1 na 2-2, mtawalia.
Mambo pia hayakuwa tofauti kati ya Villarreal na washindi wa zamani Juventus nchini Uhispania. Georges Mikautadze aliweka Villarreal kifua mbele dakika ya 18 kabla ya Juve kujibu mara mbili mapema katika kipindi cha pili kupitia kwa Federico Gatti na Francisco Conceicao.
Renato Veiga alihakikishia Villarreal alama moja aliposawazisha 2-2 dakika za majeruhi.
Dortmund walilipua Athletic Bilbao 4-1 kupitia mabao ya Daniel Svensson, Carney Chukwuemeka, Serhou Guirassy na Julian Brandt. Bilbao walijifariji kwa bao kutoka kwa Gorka Guruzeta.
Mabao ya Rasmus Hojlund anayechezea Napoli kwa mkopo kutoka Manchester United yalitosha kuzamisha Sporting 2-1 ugani Diego Armando Maradona, Italia. Luis Suarez alifungia Sporting bao la kujiliwaza.
Newcastle nao walirarua wenyeji Union Saint-Gilloise 4-0 baada ya kumwaga kipa Kjell Scherpen kupitia kwa Anthony Gordon (penalti mbili), Nick Woltemade na Harvey Barnes nchini Ubelgiji.
Katika msimamo wa Ligi hiyo ya mabingwa barani Ulaya, Bayern wanaongoza jedwali kwa alama sita kwa tofauti ya ubora wa mabao pamoja na Real Madrid, PSG, Inter Milan, Arsenal na Qarabag kwenye ligi hiyo ya klabu 36, mtawalia.
Matokeo (Oktoba 1)
Qarabag 2 Copenhagen 0, Union Saint-Gilloise 0 Newcastle 4, Monaco 2 Manchester City 2, Dortmund 4 Athletic Bilbao 1, Napoli 2 Sporting 1, Villarreal 2 Juventus 2, Arsenal 2 Olympiacos 0, Barcelona 1 PSG 2, Leverkusen 1 PSV Eindhoven 1.