Habari

Wavulana 2 wa Kisomali waliokamatwa kwa kudharau bendera ya Kenya nje kwa dhamana

Na RICHARD MUNGUTI October 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAVULANA wawili kutoka nchini Somalia waliokamatwa na kuzuiliwa kwa kuidharau bendera ya Kenya wiki iliyopita wameachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 pesa tasilimu kila mmoja.

Hakimu mwandamizi Rose Gitau anayesikiza kesi za watoto aliamuru raia wa Kenya mmoja awadhamini wavulana hao wawili wa umri wa miaka 14 na 17 mtawalia.

Bi Gitau alimkabidhi Bw Mohammed Ali, raia wa Kenya wavulana hao baada ya kueleza mahakama “ni jamaa yao na kwamba familia nyingine yao iko nchini Somalia.”

Bi Gitau aliwaachilia kwa dhamana watoto hao baada ya wakili Ishmael Nyaribo kueleza mahakama kwamba wazazi wao wamefika nchini Kenya kufuata kesi ya wanao baada ya kupashwa habari kwamba “wametiwa nguvuni kwa kuidharau bendera ya Kenya katika uwanja wa Nyayo wakati wa mechi ya kandanda.”

Hakimu alimwamuru Bw Ali awafikishe wavulana hao kortini Oktoba 8, 2025 watakaposhtakiwa kwa makosa ya kupatikana nchini Kenya bila idhini ya Idara ya Uhamiaji, kudharau bendera ya Kenya na kuvuruga amani.

“Kutokana na cheti cha mashtaka kilichowasilisha kortini na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma-DPP- Renson Ingonga- wavulana hawa wanakabiliwa na mashtaka mabaya,” Bi Gitau alisema.

Wavulana hao hawajasomewa mashtaka kwa vile idara ya watoto (CBO) na idara ya urekebishaji tabia haijawasilisha ripoti kuwahusu wavulana kubaini ikiwa ni wanafunzi, walikuwa wameingia nchini Kenya kufanya kazi gani, ikiwa ni wakimbizi na watakaa Kenya muda gani.

Hakimu aliamuru wavulana hao waachiliwe kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh50,000 kila mmoja na wadhamini wawili mmoja wao akiwa raia wa Kenya.

Wavulana hao walifikishwa kortini mara ya kwanza Septemba 26, 2025 na kuagizwa wazuiliwe katika Idara ya Watoto (CPU), kituo cha Polisi cha Gigiri, Nairobi kwa siku nne.

Walifikishwa kortini Oktoba 2, 2025 na mahakama ikaelezwa ripoti za CBO na Urekebishaji tabia haziko tayari kwa vile washukiwa hao hawajui Kiingereza wala Kiswahili.

“Karani wa mahakama anayefahamu lugha ya Kisomali atawasaidia maafisa wa idara ya watoto na urekebishaji tabia kuwatafsiria taarifa za wavulana hawa wawili,” Bi Gitau aliamuru.

Wakiwa katika kituo cha Polisi cha Gigiri-Idara ya Watoto (CPU), wawili hao aliamuru wahojiwe ibainike walikuwa wameingia nchini Kenya kufanya nini ilhali ni raia wa Somalia.

Pia aliamuru umri wa wawili hao uchunguzwe na utathminiwe na Daktari kutoka Hospitali ya Serikali.