Habari za Kitaifa

Nitanyoosha mambo; mimi ndiye tiba ya matatizo ya Kenya, asema Jaji Mstaafu Maraga

Na KEVIN CHERUIYOT October 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ALIYEKUWA Jaji Mkuu, David Maraga, amemaliza kimya cha miezi mingi kuhusu chama atakachotumia katika safari yake ya kuwania urais 2027 kwa kujiunga na chama cha United Green Movement (UGM).

Bw Maraga, ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa uongozi wa Rais William Ruto, alisema yeye ndiye tiba ya matatizo yanayokumba Wakenya chini ya utawala wa Kenya Kwanza.

Kulingana naye, chama hicho kina maadili na misingi inayolingana na falsafa yake ya uongozi unaozingatia katiba badala ya kulazimisha mambo kwa wananchi.

Akizungumza jana wakati wa kukubali rasmi wadhifa wa kiongozi wa chama hicho, Bw Maraga aliwahakikishia Wakenya kuwa ana dhamira ya kurekebisha mifumo iliyoharibika.

“Tangu nitangaze nia ya kuwania urais, Wakenya wengi wamekuwa wakiniuliza chama changu ni kipi, nami nimekuwa nikiwaambia kuwa bado natafuta. Si kazi rahisi kama wengi wanavyofikiria kupata chama kinacholingana na misingi unayoamini,” alisema Bw Maraga.

Alisema kuwa katiba ya chama hicho inaendana na ndoto yake kama Rais ajaye wa Kenya, ambayo ni kuzingatia utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa wananchi.

Iwapo atachaguliwa kuwa Rais, aliahidi kuhakikisha kuwa ushirikishaji wa umma unapewa kipaumbele katika sekta zote ili kukuza uwazi na uwajibikaji.

“Nikichaguliwa Rais wa taifa hili, nimejitolea kulijenga upya taifa letu, kurejesha utu na heshima ya Mkenya, roho ambayo si tu inajidhihirisha kwenye katiba ya chama cha Green Movement, bali pia miongoni mwa wanachama wachache na wajumbe niliokutana nao.”

Bw Maraga aliwapongeza waanzilishi wa chama, akiwemo aliyekuwa Mbunge wa Ndhiwa Neto Agostinho, kwa kumpa jukwaa la kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini.

“Jopo la waanzilishi, kama chuo cha uchaguzi cha chama, limenichagua mapema kusubiri kuteuliwa baadaye na Mkutano Mkuu wa Kitaifa kama mgombea urais wa chama cha United Green Movement katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.”

Akitambua changamoto zilizo mbele yake, aliwataka wafuasi wake na wanachama wa chama hicho kuwa na uthabiti na matumaini.

“Nitafanya kila niwezalo kukiimarisha chama hiki na kukifanya kuwa miongoni mwa vyama imara zaidi nchini. Chama ambacho kitaibuka mshindi si tu katika urais 2027, bali pia kitashinda viti vingi katika Bunge la Kitaifa na mabunge ya kaunti.”

Aliongeza kuwa, kuanzia uchaguzi mdogo wa Novemba na mipango ya kuimarisha chama, ataanza mikakati mara moja bila kusita, kwa kuandaa mikutano na wajumbe.

Bw Maraga alitangaza kuwa wikendi ijayo, atakutana na wajumbe wa kaunti za Homa Bay na Kisumu kupanga mbinu za kushinda uchaguzi mdogo wa eneobunge la Ugunja.

“Tutazindua ratiba ya mikutano katika kaunti zingine kabla ya kuzindua rasmi chama cha United Green Movement kuwa chama changu kwenye hafla ya hadhara jijini Nairobi, labda kabla ya mwisho wa mwezi huu.”

Wakati huo huo, Maraga alikosoa mabadiliko yanayotekelezwa katika sekta ya elimu na afya chini ya utawala wa Rais Ruto, akisema Wakenya watanufaika zaidi chini ya uongozi wake mnamo 2027.

“Ninaamini haya yatawahamasisha Wakenya kujiunga kwa wingi na chama cha United Green Movement na kusaidia kujenga vuguvugu la ukatiba hapa nchini, kwa sababu tumekubaliana kwamba ‘Ukatiba ndio tiba.’”

Aliendelea kusema kuwa atahakikisha matarajio ya vijana wa Kenya yanatimizwa kwa kurekebisha mifumo iliyovunjika na kuzingatia utu.

“Tutalinda haki zote za kibinadamu zilizohakikishwa kwenye katiba. Tutazingatia wajibu wa kikatiba kama kutoa huduma za afya, elimu, na kulinda mali ya wananchi.”

Kwa mujibu wa Bw Maraga, Kenya iko katika hatari ya kuwa taifa lililofeli kutokana na ukatili wa polisi dhidi ya waandamanaji wa amani.

“Sijawahi kuona nchi yoyote ambapo vyombo vya usalama vinashirikiana na wahuni.”

Katika kujenga ushirikiano wa kisiasa, alisema chama kiko tayari kushirikiana na vyama vingine vyenye misingi na maono yanayofanana.

Miongoni mwa masharti ya kushirikiana ni kujitolea kupambana na ufisadi sugu nchini.

Alikanusha madai kwamba, yeye ni mradi wa mtu fulani, akisema hana mpango wa kusikiliza wanaompinga au wanaomtaka ajiondoe katika kinyang’anyiro cha urais.

“Siogopi. Wale wanaonitishia na kunitaka niungane na mirengo yao wajue kuwa ninawania nafasi ya juu kabisa ili kulinda na kusimamia katiba ya nchi.”

Bw Maraga alipata umaarufu mkubwa baada ya kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2017.