Habari za Kaunti

Kanjo wa Siaya waadhibiwa kwa kuruhusu wahuni kupiga wauguzi waliokuwa wanaandamana

Na CHARLES WASONGA October 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI ya Kaunti ya Siaya imewatuma likizo ya lazima ya siku 30 maafisa wa idara ya ulinzi katika kaunti hiyo kufuatia kisa cha juzi ambapo wahuni waliwashambulia wauguzi waliokuwa wakiandamana nje ya afisi ya Gavana James Orengo.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Alhamisi, Oktoba 2, 2025, Katibu wa Kaunti Joseph Ogutu alisema hatua hiyo imechukuliwa “ili kutoa nafasi ya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo la kuchukiza.”

“Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na askari wote waliokuwa kazini katika makao makuu ya serikali ya kaunti wakati wa tukio hilo Jumanne wameagizwa kwenda likizo ya lazima mara moja, kutoa nafasi ya asasi za usalama kuendesha uchunguzi kuhusu tukio hilo,” akaeleza.

Askari hao wamekashifiwa kwa kufeli kuwazuia wahalifu hao, au kuchochea, kuwashambulia wauguzi hao waliokuwa wakiandamana kushinikiza walipwe malimbikizi ya mishahara na kuboreshwa kwa mazingira yao ya kazi.

Kulingana na Katibu wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi Nchini (KNUN), tawi la Siaya Kennedy Khamisi, jumla ya wauguzi 20 walijeruhiwa katika purukshani hizo.

Wengine wengi walinyang’wa simu zao wa rununu na mikoba katika fujo hizo.

Awali, wauguzi hao ambao wamekuwa wakigoma kwa zaidi ya siku 14 walifanya maandamano katika barabara za mji wa Siaya kabla ya kukongamana nje ya lango kuu la makao makuu ya kaunti ambako kuna afisi ya Gavana James Orengo.

Walinzi waliwazuia kuingia humo na hapo ndipo wakashambuliwa kwa ukatili na wahuni waliojihami kwa marungu.

“Hakuna vitisho vitakavyotuzuia kupigania haki yetu. Ni makosa kwa serikali ya kaunti kuwatuma wahalifu kuwashambulia wenzetu ambao waliokuwa wakifanya maandamano ya amani wakitaka walipwe mishahara ya miezi mitatu iliyocheleweshwa,” akasema Khamisi huku akitangaza kuwa mgomo wao utaendelea hadi wenzao walioumia watakapopata nafuu.

Alhamisi, Bw Ogutu alikashifu kushambuliwa kwa wauguzi hao akisema serikali ya kaunti ya Siaya ingependa kushughulikia malalamishi ya wafanyakazi wake kwa njia ya mazungumzo.

“Aidha, tunatoa wito kwa wauguzi na wahudumu wengine wa afya kuwasilisha malalamishi yao kupitia asasi zinazotambuliwa badala ya kuamua kuchukulia sheria mikononi mwao,” akaeleza.